Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali lawamani kushindwa kujenga Zahanati Nyampalala

Nyampalalaaa.png Serikali lawamani kushindwa kujenga Zahanati Nyampalala

Fri, 23 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwaka 2015 wakati Chama Cha Mapinduzi kikisaka ridhaa kwa wananchi, kilitangaza kujenga zanahati katika kila kijiji nchini.

Kwa mujibu wa Ilani hiyo yam waka 2015-2020, CCM iliahidi kujenga zanahati kwa kila kijiji na kuweka vifaa tiba kwa ajili ya kuwaondolea wananchi adha ya kutembea umbali mrefu, lakini pia kuthibiti vifo vinavyoweza kuepukika.

Hata hivyo, mpaka sasa wananchi wa Kijiji cha Nyampalahala kilichopo Kata ya Buziku Wilaya ya Chato mkoani Geita, hawana zahanati na wameilalamikia Serikali kwa kushindwa kukamilisha ujenzi.

Kijiji hicho chenye wakazi 4,321 hakina zanahati na wananchi walichukua jukumu la kuanzisha ujenzi wakichangishana na kutumia nguvu miaka nane iliyopita, lakini Serikali imeshindwa kusaidia kukamilisha ujenzi wake mpaka sasa na kubaki boma.

Mkuu wa Wilaya ya Chato, Deusdedith Katwale amekiri kuyasikilia malalamiko ya kutokamilika kwa zahanati hiyo mwaka jana na akaielekeza halmashauri kuhakikisha inakamilisha ujenzi huo.

Hata hivyo, naye akaeleza kushangazwa kwake na kutokamilishwa kwa zanahati hiyo mpaka sasa huku wananchi wakiendelea kuteseka.

Katwale bila kutaja takwimu akaeleza kuwa Kata ya Buziku ndiyo inaonyoongza kwa kuwa na idadi kubwa ya vifo vya wajawazito jambo alilosema halifurahishi na halistahili kufumbiwa macho.

“Inashangaza licha ya kuiagiza halmashauri kukamilisha ujenzi wa hii zahanati, lakini hakuna kilichofanyika. Maisha ya mtu ni ya thamani kubwa sana, jambo hili halifurahishi na haliwezi kuendelea kufumbiwa macho wala kusubiri,” amesema Katwale ambaye ametoa muda wa miezi nane kuanzia sasa kwa halmashauri kukamilisha ujenzi huo.

Kaimu Mganga Mkuu wa Chato, Elibariki Mollel amekiri ujenzi za zahanati hiyo kuchelewa na kusema kuwa halmashauri itapambana kutafuta fedha kukamilisha ujenzi ndani ya muda uliotolewa ili wananchi waweze kupata huduma za afya karibu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mbele ya mkuu wa wilaya huyo wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi, Mariam Elias na Fred Madirisha wamesema licha ya kukamilisha boma miaka mingi iliyopita hadi sasa ujenzi haujakamilika.

“Sisi tuna shida kubwa ya huduma za afya tulikaa kama wananchi tukakubaliana tujenge zahanati tukachimba msingi, tukasomba mawe na mchanga wenyewe na tukakubaliana kuchanga fedha za kuinua boma, lakini hakuna msaada wa wala ushiriki wa Serikali mpaka sasa. Ni miaka minane imepita sasa, halmashauri iko kimya na sio kwamba, hawafahamu hili…wanalijua,” amesema Mariam.

Amesema wanalazimika kutumia muda mrefu na gharama kubwa kufuata huduma za afya umbali na kilomita 14 kwenda Buziku. Kutokana na uwezo tofauti wa wananchi, wapo wanaotumia usafiri wa baiskeli jambo ambalo huwafanya wengine kujifungulia njiani kwa wajawazito.

“Ni miaka minane sasa kama sio tisa tumejenga hii zahanati, lakini tumekosa msaada. Watu wanakwenda kliniki na baiskeli ukisema utumie bodaboda utalipa Sh15,000 hadi Buziku na bado barabara ni mbaya. Tunaomba hili litafutiwe ufumbuzi, nguvu zimetuishia hatuna uwezo wa kukamilisha huu ujenzi,“ amesema Mariam.

Diwani wa Kata ya Buziku, Salamah Ngasa amesema moja ya changamoto ni kutokamilika kwa zahanati hiyo hivyo kuhatarisha usalama wa wananchi wake.

“Mkuu nikushukuru kwa kufika eneo hili wananchi hawa wanateseka kutafuta huduma za afya, wajawazito hawawezi kwenda kliniki na hata wakienda inawalazimu kutembea kilomita 14, hii imesababisha vifo visivyo vya lazima. Kwa mwaka huu pekee tayari wajawazito watatu wamepoteza maisha, na wagonjwa wengine hali ni mbaya kwa sababu huduma za afya ziko mbali,” amesema Diwani Ngasa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live