Serikali mkoani Mara imezindua uwekaji wa vigingi (bikoni) kati ya mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na vijiji vinavyopakana na hifadhi hiyo huku ikiwataka wanasiasa kuacha kutumia suala hilo kisisasa.
Uwekaji wa vigingi ni matokeo ya maamuzi yaliyotolewa na Baraza la Mawaziri kufuatia ushauri wa kamati ya mawaziri nane iliyoundwa na Serikali ya awaku ya tano kukusanya maoni kuhusu migogoro kati ya wananchi na hifadhi za taifa ambapo pamoja na mambo mengine ilishauri eneo kinga (buffer zone) lenye ukubwa wa mita 500 lirejeshwe kwa wananchi.
Akizungumza Machi 27, 2023 katika kijiji cha Kengonga kabla ya uzinduzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee amesema amepata taarifa kutoka kwa baadhi ya viongozi kupinga uwekeji huo wa vigingi.
“Nimepigiwa simu na Waitara anapinga uwekaji wa vigingi, mimi natekeleza maagizo ya serikali sitakubali mtu yeyote kwa nafasi yake ama cheo chake akwamishe jambo hili,nawaomba viongozi wenzangu tuheshimiane katika hili na tuwe wamoja tulikamilishe jambo hili mgogoro umedumu kwa miaka mingi sasa tuseme basi,” amesema
"Serikali inataka wananchi wanufaike zaidi na hifadhi hii na tumeambiwa hizo mita 500 zinatakiwa kutumika kwa shughuli zinazoendana na uhifadhi, tunataka wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi wawekeze hapa ili wananchi waweze kujipatia kipato waondokane na umasikini na sio migogoro tena,”
Awali Mhifadhi Mkuu wa hifadhi hiyo, Izunde Msindai amesema vijiji vitakavyohusika katika uwekaji huo wa vigingi ni pamoja na Kegonga, Nyandage, Kenyamosabi, Masanga, Karakatonga na Nyabirongo.
Amesema kuwa uwekaji huo wa vigingi utahusisha eneo lenye urefu wa kilomita 30 na kwamba mpaka huo ni kwa mujibu wa tangazo la Serikali la mwaka 1968 na si vinginevyo.
“kazi hii itafanywa na wataalmu kutoka wizara ya ardhi vingingi 162 vitawekwa na timu ya watu 69 na viongozi wa vijiji husika pia watashirikishwa na tunatarajia kuwa itakamilika ndani ya siku 30,” amesema
Katibu wa CCM Mkoa wa Mara, Lengael Akyoo amesema chama hicho kinapongeza uamuzi huo wa Serikali akidai anaamini itakuwa ni suluhisho la kudumu la mgogoro katika eneo hilo
“Hatuwezi kufanya kazi kwa kurudi nyuma sisi CCM tunaamini kwa maamuzi haya mgogoro umefika mwisho wanaopinga wao wanataka mgogoro uendelee na hatutakubali tunaomba yeyote atakayetaka kukwamisha achukuliwe hatua za kisheria, amesema Akyoo
Mkazi wa kijiji cha Kegonga, Wambura Omahe amesema umefika muda wanasiasa waache kutumia mgogoro huo kwa maslahi yao badala yake watangulize maslahi ya wananchi mbele.
“Ndugu zetu wameuwawa, mifugo yetu imeuwawa sasa kama Serikali imeona hii ndio njia sahihi basi tuunge mkono uamuzi tusitafute umaarufu wakati watu wanaumia,”amesema
Alipotafutwa Mbunge wa Tarime vijijini, Mwita Waitara amesema kuwa ataitisha mkutano na waandishi wa habari kutoa ufafanuzi juu ya suala hilo.