Shilingi bilioni 27 zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya upanuzi na ukarabati wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, mkoani Mara inatarajia kuokoa zaidi ya Shilingi milioni 720 zilizokuwa zikitumika kusafirisha wagonjwa kila mwaka ili kufuata huduma za kibingwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, na Hospitali ya Kanda, Bugando iliyopo Mwanza.
Fedha hizo zimetolewa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ili kusogeza huduma za kibingwa mkoani Mara na kufanya ukarabati, ujenzi wa majengo mapya na ununuzi wa vifaa tiba katika hospitali hiyo iliyopo Kiwangwa, Manispaa ya Musoma.
Mganga Mfawidhi Hospitali hiyo, Dkt. Osimund Dyegura amesema Sh. bilioni 27 zilizotolewa zimeboresha huduma katika hospitali kuanzia miundombinu na ubora wa huduma za utabibu ikiwemo kutibu mivunjiko ya mifupa kutokana na ajali, upasuaji wa jumla, matibabu ya watoto hasa waliozaliwa chini ya gramu 800, na huduma za kuchuja damu.