Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali kujenga machinjio bora ya kuku

43707 Pic+wabunge Serikali kujenga machinjio bora ya kuku

Tue, 26 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Serikali imejipanga kujenga machinjio ya kuku ya kisasa katika miji mikubwa ili kurahisisha upatikanaji wa kitoweo hicho.

Mbali na kufanya hivyo imeweka mikakati ya kuanzisha machinjio inayotembea ili kutoa huduma katika maeneo ya pembezoni mwa miji zikiwa ni juhudi za kuongeza sifa ya kitoweo hicho kukidhi vigezo vya kushindani kwenye masoko ya kimataifa.

Hayo yamesemwa leo, Jumatatu Februari 25, 2019 katika mkutano uliowakutanisha wadau wa ufugaji kuku pamoja na taasisi isiyo ya kiserikali ya Victoria Finance kujadili namna nzuri za utoaji mikopo kwa wafugaji wa kuku ambao wanakabiliwa na upungufu wa mtaji.

Mtafiti na mratibu wa ndege wafugwao kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk John Kaijage amesema machinjio yaliyopo sasa hayaridhishi kwa wanunuzi wa nje kununua na kutumia bidhaa hiyo.

"Tembelea tu machinjio mnayoyajua kama pale Kisutu uone jinsi hali ilivyo, hautavutiwa nayo hata kidogo. Sasa kama wewe hali ni hivyo itakuaje kwa wanunuzi wetu?" Amehoji Dk Kaijage

"Na hii tutaipendekeza katika bajeti ijayo ili tuweze kutengewa pesa na tunataka maeneo haya yawepo hadi katika kila yalipo machinjio ya ng'ombe," ameongeza.

Katibu mkuu wa chama cha wafugaji kuku nchini, Alloyce Makoye amesema kuanzishwa kwa machinjio hayo kutaongeza thamani ya bidhaa hiyo na kutaongeza uhakika wa ufugaji wa kisasa.

"Kuku watakaochinjwa watakuwa salama kwa afya kutokana na kufanyiwa vipimo, uchinjaji holela usiozingatia viwango hautakuwepo tena," amesema Makoye.

Kwa upande wake, mkurugenzi mtendaji wa Victoria Finance, Julius Mcharo amesema ili kuyafikia masoko hayo wafugaji wanatakiwa kuwa na mtaji wa kutosha, kuongeza uzalishaji na kuwa na uwezo wa kukabiliana na magonjwa.

"Ndiyo maana tumeamua kukutana nao hapa ili kupata majibu sahihi ya changamoto zao na njia sahihi za kuwapatia mikopo hiyo," amesema Mcharo.



Chanzo: mwananchi.co.tz