Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali kujenga daraja mto uliouwa wanafunzi Kigoma

Pic Vifo Mtumbwiii Serikali kujenga daraja mto uliouwa wanafunzi Kigoma

Sat, 25 Feb 2023 Chanzo: Mwananchi

Wakati miili ya wanafunzi wawili kati ya wanne waliozama ndani ya maji ya mto Luiche juzi imepatikana, Serikali imetangaza uamuzi wa kujenga daraja eneo hilo kuwaondolea wananchi adha ya kutegemea mitumbwi isiyo salama.

Uamuzi huo umetangazwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Tobias Andengenye leo Jumamosi Februari 25, 2023 wakati wa hafla fupi ya kutoa heshima za mwisho kwa miili ya wanafunzi hao iliyofanyika viwanja vya Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Kigoma, Maweni.

“Pamoja na kujenga daraja eneo la mto Luiche, Serikali pia itatekeleza miradi ya ujenzi wa meli na vivuko kwa ajili ya kusafirisha abiria na mizigo katika mwambao wa Ziwa Tanganyika,” amesema Andengenye

Hii siyo mara ya kwanza Serikali kuahidi kuenga daraja eneo la mto Luiche kwani ahadi kama hiyo imewahi kyutolewa Februari, 2021 na aliyekuwa Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), Mkoa wa Kigoma wakati huo, Issa Liyanga.

Kwa sasa, wakazi wa Kata ya Kagera iliyoko takriban umbali ya Kilometa 12 kutoka katikati ya mji wa Kigoma wanaokadiriwwa kuwa zaidi ya 9, 000 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 wanavuka mto Luiche kwa kutumia mitumbwi isiyo salama kwa gharam kati ya Sh400 hadi Sh1, 000 kwa ajili ya nauli ya mitumbwi.

Mto Luiche inayomwaga maji yake ndani ya Ziwa Tanganyika hujaa na maji yake kwenda kwa kasi nyakati za masika unapojaa huku pia ndani yake kukidaiwa kuishi wanyama wakali wakiwemo mamba na viboko

Miili kupatikana Miili ya wanafunzi wawili kati ya wanne waliozama majini baada ya mtumbwi waliopanda kupinduka imepatikana ndani ya maji ya mto Luiche, hatua chache kabla ya kuingia Ziwa Tanganyika ambako mto huo humwaga maji yake.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kigoma, Jacob Chacha ametaja wanafunzi ambao miili yao imepatikana kuwa ni Zabibu Jumanne (8) aliyekuwa anasoma darasa la pili na Ramadhani Matatizo (12) aliyekuwa darasa la tano.

“Jitihada zinaendelea kuwatafuta Tatu Omari na Ashura Ramadhani ambao hawajaonekana tangu mtumbwi ulipopinduka,” amesema Kamanda Chacha.

Wanafunzi waliofikwa mauti, wenzao wawili ambao hawajapatikana pamoja wengine wawili waliookolewa walizama majini Saa 1:30 asubuhi jana Ijumaa Februari 24, 2023 baada ya mtumbwi wao kupinduka wakati wakivuka mto Luiche wakitokea mtaa wa Mgumile kwenda Shule ya Msingi Kagera Manispaa ya Kigoma Ujiji kupinduka.

Wanafunzi wawili, Issa Omari na Michael Gogolo pamoja na nahodha wa mtumbwi, Demee Ntuguye waliokolewa katika ajali hiyo.

Gharama ya msiba Katika hatua nyingine, Serikali kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Tobia Andengenye imetangaza kugharamia shughuli zote za mazishi ya wanafunzi hao waliofikwa na mauti wakiwa njiani kwenda shuleni.

“Tumepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za ajali hii iliyopoteza maisha ya watoto wetu; Serikali inaungana na wafiwa katika msiba huu mzito na itabeba gharama zote za msiba huu kuhakikisha watoto wetu wanapumzishwa kwa heshima zote,” alisema Andengenye

Chanzo: Mwananchi