Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali kujenga daraja mto Mori vilikotokea vifo vya watu watano

Mori Sehemu ya Mto Mori

Thu, 12 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imesema tayari imeshatuma timu ya wataalamu kwenda kufanya tathmini ya ujenzi wa daraja katika mto Mori wilayani Rorya ambalo limekuwa kilio cha muda mrefu cha wananchi wa eneo hilo.

Daraja hilo litakapojengwa litaunganisha kata nne za Myathorogo, Nyabhurongo, Milale na Kigunga.

Mto huo umekuwa changamoto kwa wananchi kuvuka kutoka eneo moja kwenda eneo lingine huku vifo vikitokea kutokana na mitumbwi wanayotumia wananchi kuwavusha kuzama.

Mei 7 mwaka huu mtumbwi uliokuwa ukivusha watu kwenda katika kijiji cha Randa kata ya Kigunga kutoka Kijiji cha Kowak ulizama majini na kuuwa watu watano huku wengine watano wakinusurika.

Miili ya watu hao watano ambayo iliopolewa kwa siku tofauti baada ya mtumbwi kuzama ndani ya mto Mori inatarajiwa kuagwa na kuzikwa kwa pamoja katika mazishi leo Alhamisi Mei 12, 2022.

Akizungumzia mpango wa Serikali wa kukabiliana na changamoto hiyo, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, David Silinde amesema Serikali imesikia kilio cha wananchi cha kuhitaji daraja na kinapaswa kuangalia kwa ukaribu wake kwani wanazo taarifa za matatizo yanayotokana na kivuko kwenye mto huo.

Advertisement Ametoa kauli hiyo leo bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Rorya, Jafari Chege aliyetaka Serikali itoe majibu ya lini wanakwenda kujenga daraja katika mto Mori ambacho ni kilio cha muda mrefu.

Silinde amesema tayari timu ya watu imeshatumwa kwenda kufanya tathimini ya ujenzi wa daraja hilo kwa haraka iwezekanavyo.

 “Tulishamuagiza Meneja wa Tarura kutuma wataalamu katika eneo hilo kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa kufanya tathimini ya haraka ili tuanze mchakato wa kujenga daraja hilo,” amesema Silinde.

Kwa mujibu wa Chege daraja hilo likijengwa litaokoa maisha ya wananchi ambao wamekuwa wakipoteza maisha kila mara ikiwamo watu watano waliopoteza maisha wiki iliyopita.

Chege amesema daraja hilo litaunganisha Kata nne za Myathorogo, Nyabhurongo, Milale na Kigunga ambazo zote kiungo muhimu ni kutegemea daraja la mto Mori.

Kilio cha mbunge huyu kutaka daraja la mto Mori kimekuwa ni cha muda mrefu tangu alipoingia bungeni 2020 ambapo amekuwa akieleza namna wananchi wanavyopata tabu kwenye eneo hilo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live