Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali kujenga barabara ya Ruangwa-Kiranjeranje

9926288e13d42d831ada679b2226ec89 Serikali kujenga barabara ya Ruangwa-Kiranjeranje

Sat, 24 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema Serikali ya chama hicho imepanga kujenga barabara ya kutoka Ruangwa hadi Kiranjeranje kwa kiwango cha lami.

Alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wakazi wa vijiji na kata mbalimbali za wilaya ya Ruangwa ambako alipita kumuombea kura mgombea urais wa chama hicho Dk John Magufuli na madiwani wote wa kata hizo.

Akizungumza na wakazi hao kwa nyakati tofauti, Majaliwa alisema barabara hiyo ipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM (2020-2025) na tayari Sh bilioni 1.2 zimeshatolewa ili kufanya upembuzi yakinifu na usanifu. Barabara hiyo itawafanya wakazi hao wasilazimike kupitia Nanganga hadi Lindi wanapotaka kwenda Dar es Salaam.

"Barabara ya kutoka Ruangwa - Nanjilinji - Kiranjeranje ina urefu wa km.120. Barabara hii ukiangalia kwenye ilani yetu, utaikuta ukurasa wa 75.

“Barabara nyingine ni ya kutoka Ngongo – Mandawa – Namichiga yenye urefu wa kilometa 85 na hii ilipatiwa Sh milioni 800 na kazi ya upembuzi yakinifu imekwishakamilika, sasa kazi iliyobaki ni kutafuta fedha na kuanza ujenzi," alisema Majaliwa

Katika hatua nyingine, Majaliwa ambaye ni mbunge mteule wa Jimbo la Ruangwa, alisema katika kipindi cha miaka mitano, wilaya hiyo imepokea zaidi ya Sh bilioni 100 kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

"Haijawahi kutokea. Tangu wilaya hii ianzishwe mwaka 1995, imekuwa ikipokea fedha za maendeleo kati ya Sh bilioni tatu hadi Sh bilioni nne tu. Lakini awamu hii tumepokea Shbilioni 49.5 kwa ajili ya kazi za maendeleo na hivi karibuni Dk Magufuli alitoa Sh bilioni 59 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Nanganga- Ruangwa kwa kiwango cha lami," alisema.

Katika vijiji vyote alivyosimama na kata za Mandawa, Chikundi, Namichiga na Mbekenyera, Majaliwa amewasihi wakazi hao kuwa ifikapo Jumatano Oktoba 28 wajitokeze kwa wingi na kupiga kura za ndiyo kwa Dk Magufuli na madiwani wa CCM.

"Sisi sote ni wana-Ruangwa na kikubwa tunachotaka ni maendeleo, na maendeleo hayachagui chama. Kwani tukijenga barabara, si tutatumia wote? Fanyeni maamuzi sahihi kwa kukichagua Chama Cha Mapinduzi na kumpa kura nyingi Dk John Pombe Joseph Magufuli," alisisitiza.

Wakati huohuo, Majaliwa alitumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi wa Ruangwa kwa kumpitisha bila kupingwa wakati akiwania ubunge wa jimbo hilo. Bado anaendelea na ziara yake kwenye jimbo la Ruangwa.

Chanzo: habarileo.co.tz