Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serengeti wanafunzi wote waliochaguliwa Sekondari kuanza masomo

Serengeti wanafunzi wote waliochaguliwa Sekondari kuanza masomo

Sun, 5 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Serengeti. Wanafunzi 5,238 Wilayani Serengeti Mkoani Mara Tanzania, wanatarajiwa kuanza masomo yao kesho Januari 6, 2020, baada ya maandalizi kukamilika.

Wanafunzi hao ni wale waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza baada ya kuhitimu masomo yao ya shule ya msingi na kufaulu mtihani wa Taifa mwaka jana 2019.

Mkoa wa Mara ni miongoni mwa mikoa kumi inayokabiliwa na upungufu wa vyumba vya madarasa na kusababisha wanafunzi 9,493 waliofaulu kukosa nafasi za kuanza masomo kesho shule zinapofunguliwa.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Juma Hamsini akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Januari 5, 2020, amesema wanafunzi 735 waliokuwa wamekosa nafasi wilayani humo wamepata nafasi kwenye shule 32.

“Wanafunzi 5,238 walifaulu, lakini waliokuwa wamepata nafasi ni 4,503, wanafunzi 735 wakawa wamebaki, lakini tulikuwa na vyumba vingi vilikuwa havijakamilika sawasawa lakini sasa vimekamilika, hivyo wataanza  siku moja wote na taarifa zimeishasambazwa maeneo yote ya wilayani,” amesema.

Amesema wasichana 70 waliokuwa wamechaguliwa shule za kutwa, wamewapeleka shule za bweni za sekondari za Robanda, Kisangura na Ikoma ili kuwawezesha kusoma katika mazingira rafiki.

Mkuu wa wilaya hiyo, Nurdin Babu amesema kuna shule tatu mpya wanategemea kuzifungua mwezi ujao, baadhi ya wanafunzi watahamishiwa huko.

“Tunategemea kufungua sekondari za Ngarawani, Musati na Gesarya ambazo wanafunzi ambao kwa sasa watakuwa wanatoka maeneo hayo kwenda shule kama Nyamoko na Ikorongo watahamishiwa huko kwa kuwa ni maeneo ya jirani na wanakotoka,” amesema Babu.

Amesema kila mwaka wanajitahidi kufungua sekondari mpya, ndiyo maana hawapati shida sana kubwa ya uhaba wa vyumba vya madarasa.

“Tunaendelea na ujenzi wa sekondari ya Nyerere katika Kata ya Mugumu ambayo mwakani itachukua wanafunzi, mwaka jana tumefungua shule mpya tano za sekondari, hii ni juhudi za wananchi, halmashauri, Serikali Kuu na wadau wengine, kwa sasa tunapambana na ujenzi wa nyumba za walimu katika shule hizo,” amesema mkuu huyo wa wilaya.

Desemba 5, 2019, Waziri wa Tamisemi Selemani Jafo akizungumzia wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza, aliwataka wakuu wa mikoa kukamilisha ujenzi wa madarasa ifikapo Februari 29, 2020 ili kuwezesha wanafunzi 30,132 waliochaguliwa na kukosa nafasi za kuanza masomo kutokana na uhaba wa madarasa waweze kuanza masomo yao.

Hata hivyo, Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa Desemba 2019  aliagiza wakuu wa mikoa kusimamia ipasavyo ujenzi huo ili watoto waliochaguliwa waweze kuanza masomo  kwa pamoja.

Chanzo: mwananchi.co.tz