Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sendeka akataa kukubali maelezo ya mama anayedai kumla mtoto

85603 Pic+mama Sendeka akataa kukubali maelezo ya mama anayedai kumla mtoto

Sun, 24 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Njombe. IMama ambaye amedai kumchinja mtoto wake, kuchemsha nyama yake na baadaye kuila, amedai alifanya hivyo baada ya kugombana na mumewe, lakini mkuu wa mkoa wa Njombe hajakubaliana na maelezo hayo.

Badala yake, mkuu huyo, Christopher Ole Sendeka ameagiza Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina kujua kilichotokea, akisema maelezo mepesi, mafupi na ya mtu mmoja hayawezi kutoa picha nzima ya tukio hilo.

Mama huyo, Christina Mlelwa anadaiwa kufanya tendo hilo Novemba 18, saa 12:00 jioni, alipomchinja mwanaye aitwaye Joseph Gumbilo (4), ambaye alikuwa mlemavu wa viungo.

Mama huyo, 38, anadai kuwa alifanya uamuzi huo baada ya kugombana na mume wake anayefahamika kwa jina la Daniel Gumbilo. Wote wawili ni wakazi wa kijiji cha Mavanga wilayani Ludewa, Njombe.

Akizungumza lugha ya Kipangwa, Christina alisema siku hiyo aligombana na mumewe na hivyo kupata na hasira.

“Nilikuwa nagombana na mume wangu. Katika kugombana naye hasira ikanibana ndio nikaamua kufanya hivyo,” alisema Christina.

Baada ya kumuua, alienda kutumbukiza mabaki ya viungo katika choo kilichopo karibu na kichaka kilichopo pembezoni mwa nyumba yake.

Naye Gumbilo aliiambia Mwananchi kuwa mkewe aliwahi kujaribu kufanya tukio kama hilo kwa mtoto wake mwingine anayesoma, lakini hakufanikiwa.

“Huyu mwenzangu nashindwa kumuelewa kwa sababu hata huko nyuma aliwahi kutaka kumua mwanangu ambaye hivi sasa yupo shuleni” alisema Daniel.

Mmoja wa majirani, Bruno Mkorongo alisema siku ya tukio mume wa Christina alitoa taarifa kwa uongozi wa kijiji kuwa mtoto haonekani ndipo waposaidiana naye kumtafuta.

“Baada ya kutoa taarifa hiyo viongozi wa serikali wakaenda hadi nyumbani kwa yule mama. Wakati wanamuhoji alieleza kwamba amemficha mtoto na amekula nyama yake,” alisema Bruno.

“Kwa kweli tulikuwa tunaishi naye kama jirani mwema na maisha yao walikuwa wanaishi vizuri tu, lakini tunashangaa kwa tukio kama hili.”

Alisema mama huyo aliwaambia kuwa nyama nyingine ya mtoto wake ametumbukiza chooni na kwa sababu ilikuwa giza, hawakuona mabaki yoyote.

Walipoendelea kumuhoji, aliwajibu kuwa ametupa porini hivyo asubuhi mtendaji aliongozana na mgambo kwenda eneo hilo na kukuta miguu ya huyo mtoto na kichwa,ngozi na utumbo.

Lakini mkuu wa mkoa, Christopher Ole Sendeka, ambaye alikuwa na kamati ya ulinzi na usalama, hakuridhika na maelezo hayo.

“Majibu mepesi na maelezo mafupi ya mtu ambaye inaonekana akili yake si timamu, hayawezi kuwa ndio jawabu la jumla la hali ya tukio hili,” alisema Sendeka.

“Naagiza RPC tumia utaalamu wako na wasaidizi wako kujua undani wa jambo hili.”

Alisema endapo wananchi hawatoi ushirikiano katika uchunguzi, awakamate wote wa kitongoji cha Mji Mwema.

Kamanda wa polisi wa mkoa, Khamis Issa alisema wanaendelea na uchunguzi ili wahusika wachukuliwe hatua.

“jambo hili ni zito haliwezi kuwa na majibu mepese. Litakuwa na majibu mazito na sisi kwa kutumia sheria tutahakikisha jambo hili tumelishughulikia,” alisema.

Mpaka muda huu mtuhumiwa anashikiliwa na jeshi la polisi kwa uchunguzi wa kina.

Chanzo: mwananchi.co.tz