Mahudhurio hafifu ya wanafunzi yanayotajwa kusababishwa na umbali mrefu yamepatiwa mwarobaini baada ya Serikali kukamilisha mradi wa ujenzi wa mabweni uliogharimu Sh200 milioni katika shule ya Sekondari Keni, iliyopo Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro.
Mabweni hayo ni moja kati ya miradi nane iliyotembelewa, kukaguliwa na kuwekwa jiwe la Msingi na kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa, Abdallah Shaimu Kaim ambapo thamani ya jumla ya miradi hiyo ni zaidi ya Sh700 milioni.
Akitoa taarifa ya mradi huo wa mabweni kwa kiongozi wa mbio za Mwenge, Mkuu wa Shule ya Keni, Renatus Lyimo amesema kukamilika kwa bweni hilo kutawezesha mazingira rafiki, tulivu na kuimarisha mahudhurio kwa wanafunzi.
"Mradi wa ujenzi wa bweni hili la wanafunzi wa kidato cha tano na sita ambalo litabeba wanafunzi 80 ulilenga kuboresha mazingira mazuri ya kujifunzia, kufundishia na kutawezesha mazingira rafiki na yenye utulivu ambayo yataimarisha mahudhurio kwa wanafunzi na kupunguza changamoto ya utoro," amesema Mwalimu Lyimo.
Akizungumza mara baada ya kukagua bweni hilo kiongozi huyo wa mbio za Mwenge, amewataka viongozi wa wilaya hiyo kuendelea kusimamia miradi inayotekelezwa na serikali kwa ubora na kwa viwango vinavyotakiwa kulingana na fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi hiyo.
"Baada ya kufanya ukaguzi wa kina wa nyaraka, tumejiridhisha nyaraka zote zipo vizuri, tunaamini na tunatambua mradi bado unaendelea, ninachotaka kusisitiza ni usimamizi mzuri na kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati ukiwa na ubora na viwango vinavyotakiwa lengo ni kuleta tija katika kutimiza malengo ya Watanzania wote,"amesema
Kwa upande mwingine, baadhi ya wananchi wa wilaya hiyo, wameishukuru Serikali na kwamba ni kilio cha miaka mingi kwa kuwa watoto wao wamekuwa wakitembea umbali mrefu na wakati mwingine usalama wao kuwa hatarini.
Cesilia Kavishe, Mkazi wa wilaya hiyo amesema: "Watoto wetu wamekuwa wakitaabika sana kwa muda mrefu unakuta mtoto anatembea kilomita 10 kwa siku na hii imesababisha baadhi ya watoto kukata tamaa ya kusoma, tunashukuru sana tumeletewa mabweni watoto wetu watapata ahueni na tunaamini watasoma sasa, maana tarafa mzima kulikuwa hakuna shule ya kulala,"