Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sehemu hoteli ya Ilboru Safari Lodge yaungua

46353 Pic+moto Sehemu hoteli ya Ilboru Safari Lodge yaungua

Tue, 12 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Sehemu ya hotel ya  kitalii ya Ilboru Safari Lodge na nyumba mbili zilizopo ndani ya eneo la hoteli hiyo jijini Arusha, leo, Jumanne, Machi 12,2019 zimeteketea kwa moto na kusababisha hasara ya mamilioni ya fedha ambapo chanzo chake bado hakijajulikana.

Hoteli hiyo, mali ya Kanali mstaafu Mika Metili  ilianza kuungua saa tatu na nusu asubuhi na kuvuta umati wa watu na majirani katika eneo hilo lililopo Kitongoji  cha Olitelelei, Kata ya  Ilboru wilayani Arumeru.

Meneja wa hoteli hiyo, Eddy Jask amesema wakati moto unatokea alikuwa ofisini na aliletewa taarifa na mfanyakazi kuwa moto unawaka katika nyumba kubwa anayoishi  mtoto wa mwenye hoteli pamoja na mkewe.

Jask amesema baada ya moto huo kuwaka katika nyumba hizo, ulihamia katika eneo la hoteli na kuunguza vyumba viwili na hawajui chanzo chake, lakini wanahisi itakuwa ni hitilafu ya umeme.

Akizungumzia ajali hiyo, mmoja wa wafanyakazi wa hoteli hiyo, Nelson Mushi amesema aliona moshi unatokea kwenye  nyumba kubwa ndani ya eneo na hoteli hiyo.

Amesema aliposogea alikutana na wafanyakazi wenzake wakiwa wanahangaika kutaka kuzima moto huo.

“Kama ilivyo kawaida moto ukiwa unawaka milango inajifunga na tulijaribu  kuvunja dirisha wakati  wengine wakiendelea kupiga kelele kwa kutoa taarifa kwa  watu pamoja na zimamoto ambao ndio walifika kusaidia kuzima,”amesema.

Mlinzi wa zamu wa hoteli hiyo, Adela Mwenda  amesema awali jitihada za kuzima haraka moto huo zilikwama kutokana na kuwaka kwa kasi.

“Moto ulipozidi nilienda kupiga ‘alamu’ ya usalama na tukaanza kupiga simu ndani, hakukuwa na mtu yeyote,” amesema.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ilboru, Tuwati Sukuriati  amesema alipata taarifa ya moto huo alipopigiwa simu na mmoja ya wajumbe wanaohusika na mambo ya usalama.



Chanzo: mwananchi.co.tz