Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Samia atoa Tsh.mil 470 kuunga mkono ujenzi wa Sekondari Itende

Da9a37dd55194569941f3810d2af926b.jpeg Samia atoa Tsh.mil 470 kuunga mkono ujenzi wa Sekondari Itende

Sat, 1 Jan 2022 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SHilingi milioni 470 zimetolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya Sekondari ya Kata ya Itende iliyopo jijini Mbeya ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za wananchi wa kata hiyo walioanzisha ujenzi wa shule hiyo awali kwa nguvu zao binafsi.

Wakazi wa kata hiyo waliona umuhimu wa kujenga shule ya sekondari kwenye eneo lao baada ya kuchoshwa na adha ya watoto wanaofaulu kutoka kwenye shule za msingi zilizopo kwenye kata hiyo kupangiwa shule za sekondari zilizopo katika kata nyingine na hivyo kuwalazimu kutembea umbali mrefu kufuata huduma za masomo.

Mbunge wa Mbeya Mjini na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson jana alikabidhi fedha zilizotolewa na Rais Samia kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kata ya Itende ukihudhuriwa na wananchi pamoja na wadau mbalimbali.

Kwa mujibu wa Dk Tulia, juhudi za wananchi zimefanya Rais Samia kuunga mkono maono yao hivyo kiasi cha fedha kilichotolewa ni kwa ajili ya ujenzi wa vyumba nane vya madarasa, vyoo vyenye jumla ya matundu 20, matangi mawili ya maji lita elfu kumi, maabara za sayansi tatu, ofisi za walimu na miundombinu mingine.

Akikabidhi fedha hizo, Dk Tulia Ackson alimpongeza Rais Samia kwa moyo wake wa upendo kwa wakazi wa kata hiyo pamoja na wananchi wote wa jimbo la Mbeya akisema amekuwa kiongozi msikivu na mwenye kujali shida za wananchi na kutosita kuwashika mkono wale wanaoonesha uthubutu kwenye mambo ya maendeleo.

Mbunge huyo alisema yeye binafsi kiu yake ni kuona Jiji la Mbeya linakuwa na shule bora ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi pia kusogeza huduma karibu ya wananchi.

Dk Tulia alisema shule hiyo ni majibu ya ahadi kwa wananchi wa Itende ambao walikuwa wakichangia shule jirani huu ukiwa ni ufuatiliaji wa karibu wa Diwani wa Kata ya Itende, Julius Mendagalile.

Aidha, alipongeza ushirikiano wa wananchi ambapo kwa kushirikiana na wadau wamewezesha kupatikana kwa mabati ya kuezekea majengo ya madarasa na la ofisi ya walimu.

“Mimi ni Mbunge wa kujiongeza hivyo tunapaswa kushirikiana ili kuhakikisha tunawawezesha watoto kuanza masomo mwezi Januari mwakani,” amesema Dk Tulia.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Amede Ngw’anidako aliwahakikishia wananchi kuwa taratibu za usajili wa shule hiyo zinaendelea na kwamba wanafunzi wote waliofaulu wataanza masomo Januari hii.

Chanzo: www.habarileo.co.tz