Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sakata la wizi wa gari, polisi atoa ushahidi upande wa mshitakiwa

Ceo D . Law Sakata la wizi wa gari, polisi atoa ushahidi upande wa mshitakiwa

Sun, 25 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Sakata la wizi wa gari aina ya RAV4 lenye namba za usajili T. 984 BPG, limeendelea kuibua mapya katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, baada ya askari polisi J 212 PC Damas kutoka Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni kutoa ushahidi akiwa upande wa mshtakiwa.

Wakati Damas anatoa ushahidi wake kwa kumtetea mshtakiwa Salum Mshana, tayari baadhi ya askari, akiwamo mpelelezi wa kesi hiyo walishatoa ushahidi wao kwa upande wa mashtaka kwa lengo la kuthibitisha wizi wa gari hilo.

Hali hiyo ilitokea juzi mbele ya Hakimu Mkazi, Aaron Lyamuya wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya usikilizwaji wa mashahidi wa upande wa mashtaka, ndipo askari huyo alipopanda katika kizimba cha shahidi.

“Sijawahi kukutana na kitu kama hiki - polisi kuja kuzungumza kwa upande wa utetezi. Siyo kusema kwamba inakatazwa, hapana! Inaruhusiwa kabisa.

“Haya, sawa ngoja tumsikilize. Sasa sijui utazungumza nini wakati wenzako walishazungumza kwa upande wa mashtaka. Haya mwapishe tuanze,” alisema Hakimu Lyamuya.

Akitoa ushahidi wake, akiongozwa na Wakili wa Mshtakiwa, Constantine Kakula, Damas alidai kuwa yeye anatoka ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Kitengo cha Masijala Dawati la Malalamiko.

Alidai kuwa kabla ya Aprili 17 mwaka huu, walipokea barua ya malalamiko kutoka kwa Salum ikieleza kuwa kuna mtu anatumia gari hilo wakati siyo lake. Wakaanza kulifanyia kazi kwa kuandika barua Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

“Tuliandika barua TRA ili kujua nani mmiliki wa gari hili. Majibu yalirudi kwamba mmiliki wa awali ni Victoria Njau na wa sasa ni Clerance, jina lake la pili nimelisahau kidogo.

“Baada ya taarifa hizo, tulianza kuchunguza Clerance anaishi wapi. Tulibaini anaishi Goba, Dar es Salaam. Tulikwenda kwake tukajitambulisha kuwa sisi ni maofisa wa polisi, tukamwuliza ‘kuna gari ambalo unatumia sio lako?’ Akajibu ni kweli,” alidai Damas.

Baada ya taarifa hiyo, Damas alidai waliondoka na Clerance pamoja na gari hilo lenye namba za usajili T 984 BPG hadi Kituo cha Polisi Oysterbay.

“Nilitaka kuja nalo hapa lakini ni bovu, lilishindwa kuwaka, ila nikipewa muda nitalileta,” alidai.

Hakimu Lyamula alimweleza kwamba kabla ya siku ya Ijumaa, awe amelifikisha gari hilo kwenye viwanja vya mahakama ili Jumatatu wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo liwapo kwa ajili ya kuliangalia kama ndiyo alilolielezea mbele ya mahakama ndipo aombe litolewe kama kielelezo.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Juni 19 mwaka huu kwa kuendelea kusikilizwa. Gari analodaiwa mshtakiwa Salum kuwa ameliiba ndiyo alilokutwa nalo Clerance ambapo umiliki ulibadilishwa kutoka kwa Njau kwenda kwa Clerance Oktoba 25, 2022.

Katika hati ya mashtaka, mfanyabiashara huyo anatuhumiwa kuwa Oktoba 21, 2015, akiwa eneo la Ubungo External, aliiba gari aina ya RAV4 T 984 BPG, mali ya Victoria Njau ambalo alikuwa ameaminiwa na Peter Sanga kwa ajili ya biashara.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live