Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sakata la wafanyakazi 380 wa maua lachukua sura mpya

8c2efec0367fd7ea992d7fa45be16f3a Sakata la wafanyakazi 380 wa maua lachukua sura mpya

Mon, 8 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

SAKATA la wafanyakazi 380 wa Shamba la Maua la Mount Meru Flowers lililopo wilayani Arumeru mkoani Arusha, limechukua sura mpya, baada ya viongozi wa Chama cha Wafanyakazi Mashambani (TPAWU) Kanda ya Kaskazini kuingilia kati.

Viongozi hao wa TPAWU wamefungua shauri la mgogoro katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), kutokana na mmiliki wa shamba hilo kugoma kutoa barua za kuwaachisha kazi wafanyakazi hao na kukaidi kuwalipa stahiki zao.

CMA ni idara ya Serikali na kazi yake ni kusikiliza, kusuluhisha na kuamua migogoro ya kazi; na hufanya usuluhishi kati ya mwajiri na mwajiriwa pale migogoro ya kikazi inapojitokeza. Wafanyakazi hao waliachishwa kazi Januari 29 mwaka huu huku wakidai mishahara ya miezi mitano.

Uongozi wa Kampuni ya Maua ya Mount Meru Flowers umekuwa ukikiri kuwaachisha wafanyakazi hao kazi bila ya kuwalipa stahiki zao, kwa madai kuwa kampuni imefilisika.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, Katibu wa TPAWU Kanda ya Kaskazini, Cecilia Mariwa alisema kuwa wamekaa mezani na uongozi wa shamba hilo, akiwemo Mkurugenzi Mtendaji, Lucy Urio kujua hatma ya wafanyakazi hao.

Lakini, alisema majibu ya viongozi hao ni kuwa hawana fedha ya kuwalipa wafanyakazi hao wala hawawezi kuwaandikia barua ya kuwaachisha kazi.

Mariwa alisema hatua aliyochukua Urio ya kuwaachisha kazi wafanyakazi hao 380 bila kuwapa nakala ya barua ya kusitisha ajira zao na bila kuwapa stahiki zao, sio utaratibu wa kisheria.

Alisema TPAWU imelazimika kufuata taratibu za kisheria, ikiwemo kufungua mgogoro wa kisheria CMA Mkoani Arusha ili wafanyakazi hao walipwe stahiki zao kwa mujibu wa sheria.

‘’Huwezi kumwachisha mfanyakazi bila kumpa nakala ya barua ya kusitisha ajira yake na pia bila hata kumpa stahiki zake anazodai.

Hii haijawahi kutokea, lazima tuchukue hatua kwa waajiri kama hao ‘’ alisema Mariwa. Mwanasheria wa Kampuni ya Mount Meru Flowers, Sindato Shao alikiri kuachishwa wafanyakazi hao bila kulipwa stahiki zao wala kupewa nakala ya barua ya kusitishiwa ajira zao.

Alisema kuwa mwenye kuweza kufafanua hilo ni mkurugenzi mtendaji mwenyewe na sio yeye. Shao alisema kampuni imesitisha ajira, kwa kuwa shamba hilo kwa sasa halizalishi maua na wako katika hasara kubwa na wameamua kusitisha kila kitu katika kampuni hiyo kwa sasa kwa watu wote.

Hata hivyo, wakati Mount Meru Flowers imeamua kuachisha wafanyakazi 380 bila kuwalipa stahiki zao, habari za ndani zinasema kuwa kampuni hiyo imeamua kuajiri wafanyakazi kuendelea kufanya kazi hatua ambayo imeelezwa ni kitendo cha kukwepa kulipa kodi ya serikali.

Akizungumza katika ofisi za gazeti hili, Mwenyekiti wa TPAWU wa shamba hilo, Hamza Mdemeka alisema kuwa wafanyakazi wote kwa sasa wameamua kupiga kambi katika geti la shamba hilo hadi hapo watakapopata stahiki zao.

Mdemeka alisema hatua ya viongozi wa shamba hilo kusema hawana fedha sio ya kweli, kwani kwa sasa wafanyakazi hao wanaona watu wanaingia getini na kutoka na wanapata ajira za muda.

Alidai hatua ya viongozi hao kusitisha ajira hizo, inatokana na kulimbikiza madeni ya wafanyakazi, ikiwemo mishahara na makato ya NSSF na kodi zingine za serikali.

Chanzo: habarileo.co.tz