Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sakata la ajali ya Precision Air matumbo joto

Operanews1668426826731 Sakata la ajali ya Precision Air matumbo joto

Mon, 14 Nov 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wito wa dharura wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa Baraza la Mawaziri kujadili ajali ya ndege ya Shirika la Precision Air unatarajiwa kutoa jawabu la mifumo duni ya uokoaji inayolalamikiwa huku ukiwaweka matumbo joto baadhi ya vigogo serikalini.

Hali inatajwa kuwakumba watendaji waliopaswa kuwajibika moja kwa moja katika suala la uokoaji ambalo kwa kiwango kikubwa lilizianika taasisi kadhaa za Serikali na kulaumiwa kwa uzembe.

Ndege hiyo ilianguka katika Ziwa Victoria takribani mita 100 kutoka Uwanja wa Ndege wa Bukoba, mkoani Kagera ikiwa na watu 43 waliokuwa wakitoa jijini Dar es Salaam, kati yao 39 wakiwa abiria, marubani wawili na wahudumu wawili.

Baada ya ajali hiyo iliyotokea Novemba 6, mwaka huu saa 2:53 asubuhi, shughuli za uokoaji kwa sehemu kubwa zilifanywa na wavuvi wakiongozwa na kijana Jackson Majaliwa na wenzake waliowezesha watu 24 kuokolewa.

Majaliwa ametambuliwa kama shujaa kwa shughuli hiyo na Rais Samia akaagiza aajiriwe katika Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

Wakosoaji waliozungumza na gazeti hili walisema kulikuwa na haja ya kuwepo vikosi na vifaa vya uokoaji katika ukanda wa Ziwa Victoria kutokana na kuwepo shughuli za majini na ajali kubwa zilizowahi kutokea eneo hilo.

Baadhi waliwataka walio kwenye dhamana ambao kwa namna moja au nyingine, maeneo wanayoyasimamia au kuyaongoza yalishindwa kujitokeza wakati wa uokoaji, kuwajibishwa au kujipima wenyewe na kuchukua hatua.

Katikati ya hayo, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) ilizungumza na wanahabari ikijiweka kando na ajali hiyo, ikitaka kipaumbele kitolewe kwa uchunguzi unaoendelea.

Kauli hizo ni sawa na zilizotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila pamoja na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ambao kwa nyakati tofauti walilieleza gazeti hili kwamba uchunguzi unaendelea wa ajali hiyo.

Wakati uchunguzi ukiendelea, juzi, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Zuhura Yunus akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu ziara ya Rais Samia nchini China na Misri, alitoa pole kufuatia ajali hiyo kisha akasema Rais Samia ameitisha kikao cha dharura cha baraza la mawaziri.

“Kwa taarifa tu, kutakuwa na mkutano wa dharura siku ya Jumatatu (leo) jijini Dodoma utakaojadili zaidi janga hilo,” alisema Zuhura.

Hata hivyo, alipotakiwa kufafanua zaidi kuhusu mkutano huo, Zuhura alibainisha mkutano huo ni wa Baraza la Mawaziri utakaoongozwa na Rais Samia.

“Huu ni mkutano wa baraza la mawaziri, watakutana Jumatatu kama nilivyosema na watajadili hili janga la ajali ya ndege,” alisisitiza Zuhura.

Taarifa za kuitishwa kwa kikao hicho kutangazwa mapema isivyo kawaida, zinaweza kuwa zinawaweka katika wakati mgumu viongozi mbalimbali kwenye sekta hiyo hasa ikizingatiwa, katika kipindi cha miaka ya karibuni, baraza hilo limekuwa linakutana kimyakimya.

Wadadisi wa masuala ya siasa wanaeleza, huenda kikao hicho kikatoka na uamuzi mgumu hasa ikizingatiwa, njia za uokoaji zimeelezwa kusababisha vifo vya watu hao 19 ambao endapo uokozi ungefanyika haraka huenda vifo hivyo vingepungua.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Cosmas Mnyanyi aliyezungumza na Mwananchi, alisema madhara yaliyoonekana kutokana na ajali hiyo yanaonyesha tatizo ama kwenye uwanja wa ndege au watumishi walioajiriwa kwa uokoaji.

Alieleza kikao hicho kinapaswa kuja na majawabu ya changamoto hiyo ili linapotokea tatizo wakati mwingine, kuwepo na uokoaji wa haraka.

“Lakini tunapaswa kutathmini kwamba vifaa gani tunavyo kwenye viwanja vyetu na vingapi vinafanya kazi ili tuwe tumejiandaa mapema iwapo tatizo litatokea tuwe na uwezo wa kukabiliana nalo,” alisema.

Huenda kilichotokea kinahusisha uzembe wa mamlaka fulani, lakini alisema ni vigumu kueleza moja kwa moja kwamba kuna hatua zitachukuliwa dhidi yao, kwani haijulikani sababu za kina za kilichotokea.

Maoni ya Dk Mnyanyi yanaungwa mkono na Katibu wa Chama cha Marubani Tanzania (Tapa), Kapteni Khalid Iqbal aliyekwenda mbali akisema ni muhimu mabadiliko yafanyike ya kuwapa nafasi wenye uzoefu.

“Nchi nyingi zimeajiri makamanda wastaafu wakiwemo marubani na wahandisi wenye uzoefu zaidi ya miaka 30 hadi 40 katika sekta hiyo. Mama (Rais Samia) afanye mageuzi kama aliyoyafanya katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA),” alisema.

Wazoefu hao, alisema wana ujuzi wa mambo mengi akisisitiza watendaji wakuu wa sekta ya anga hawapaswi kuchaguliwa kisiasa kuliongoza eneo hilo nyeti.

“Mageuzi makubwa yanapaswa kufanywa bila kuchelewa kwa sababu tuna wataalamu wa kutosha waliostaafu wenye umri wa miaka 60 na zaidi ambao wamebobea katika sekta hiyo,” alisema Iqbal.

‘Tuonyeshe kujifunza’

James Mbatia, mwanasiasa na mtaalamu wa majanga, alisema pamoja na mambo mengine katika kikao hicho mkuu huyo wa nchi anapaswa kuridhia kuanzishwa kwa wakala wa usimamizi wa majanga.

“Mei 11, 2015 Rais mstaafu, Jakaya Kikwete alisaini sheria ya kuanzishwa kwa wakala huo baada ya kupitia michakato yote ya kuanzishwa ikiwemo kupitishwa bungeni,” alieleza Mbatia.

Mbatia ambaye ni Mwenyekiti wa zamani wa NCCR-Mageuzi, alibainisha ni miaka saba hadi sasa pamoja na hatua zote wakala huo haukuanzishwa kwa kile kinachoelezwa na mamlaka kuwa sheria yake inapitiwa upya.

Hakuna sababu tena ya kuunda kamati yanapotokea majanga, badala yake wakala huo uanzishwe kutoa jawabu la kila janga, akisisitiza kuwa ni vema kuanza na kilichopo na kama ni marekebisho yatafanyika kwa kadri changamoto zitakapoonekana.

“Tukio la ajali ya Precision Air limeamsha hasira za Watanzania na kilichofanywa na Rais Samia ni kama kuonyesha kwamba Serikali inachukua hatua, lakini hatutadanganyika tena tunataka chombo na tukifanyie kazi,” alisema.

Umuhimu wa kuanzishwa kwa wakala huo, alisema unatokana na uzoefu wa ufanisi duni uliojitokeza katika kamati na tume mbalimbali zilizoundwa kushughulikia majanga.

“Kila ajali inaundiwa tume, kuna tume ya Mv Bukoba, tume ya Mv Spice 2011, tuna ripoti ya tume ya Mv Nyerere 2018, tuna ripoti ya jengo lililoanguka Dar es Salaam, ripoti zipo nyingi hatuhitaji tena tume zimetosha.

“Tunapoteza fedha za Watanzania, hatuhitaji tume twende kwenye vitendo tuache maneno,” alisema.

Alisema kwa sasa Ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha maafa kinahusika na kuratibu shughuli baada ya tukio, mathalan kuzika au kusafirisha miili, lakini si kuokoa.

Hatua ya kusuasua uanzishwaji wa wakala huo, Mbatia alisema inasababishwa na kukosekana utashi wa kisiasa.

Mara baada ya ajali hiyo, Taasisi ya wanasheria wa mazingira (LEAT) ilitoa taarifa kwa umma ikieleza imeshtushwa na kusikitishwa na uwezo na udhaifu wa vyombo vya uokozi vya Tanzania kwamba haikutarajiwa kwa miaka 26 tangu ajali ya MV Bukoba, vyombo hivyo havikuboreshewa utendaji wake.

“Ukweli ni kuwa vyombo na mamlaka husika zimezembea kwa kiwango cha aibu kwa taifa. Wakuu wavyo wote wawajibike na wakisita wawajibishwe mara moja,” ilisema LEAT.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live