Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sakata la Tito Magoti bado kitendawili laivuruga polisi

Mon, 23 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ikipanga leo kuzungumzia kumshikilia ofisa wa kitengo cha elimu kwa umma wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Tito Magoti, waajiri wake wamesema wataidai dhamana kwa njia ya kisheria.

Uamuzi wa LHRC unakuja ikiwa zimepita siku tatu pasipo kujua mfanyakazi wake anashikiliwa kituo gani licha ya kumtafuta katika vituo zaidi ya vitano kikiwamo kituo kikuu cha kanda hiyo bila mafanikio.

Magoti alichukuliwa Ijumaa iliyopita asubuhi na watu wasiojulikana wakiwa wamevalia kiraia eneo la Mwenge lakini jioni ya siku hiyo, Kamanda wa Polisi wa Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alitoa taarifa akisema wanamshikilia pamoja na watu wengine watatu kwa uchunguzi wa tuhuma za jinai.

Baada ya LHRC kumtafuta bila mafanikio, Mwananchi lilimtafuta jana Mambosasa kujua alipo Magoti lakini alisema yupo kituo cha polisi na leo watatoa taarifa kuhusu suala hilo.

Awali, asubuhi LHRC na familia ya Magoti walizungumza na waandishi wa habari kuhusu suala hilo. Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Anna Henga alisema polisi wanatakiwa wampatie dhamana ofisa huyo kwani ni haki yake ya msingi licha ya kutoeleza ni kituo gani cha polisi alipo.

Henga alisema kwa mujibu wa sheria mtu akikaa kituo cha polisi saa 24 anatakiwa kupatiwa dhamana au kufikishwa mahakamani, lakini imeshindikana na haijulikani alipo.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
“Kwa muktadha huu wa haki za binadamu kitendo hiki ni kibaya, kwa sababu kama huyu anafanya kazi katika kituo chakutetea haki za binadamu amefanyiwa hivi, je raia wa kawaida hali si itakuwa mbaya zaidi?” alihoji Henga.

Magoti Edwin, ambaye ni kaka wa Tito alisema familia imesikitishwa na tukio hilo ambalo limegubikwa na sintofahamu kuanzia kukamatwa kwake hadi alipo sasa.

“Mwanzoni tulipopata taarifa ametekwa tulipata hofu lakini baadaye tukapata matumaini tulipoambiwa kuwa amekamatwa na polisi, ila sasa hofu imerudi tena kwani pamoja na kuambiwa kuwa amekamatwa polisi hawakusema yupo kituo gani,” alisema. Alisema Magoti hakuwahi kueleza kuwa ana ugomvi na mtu au kuna mtu anamfuatilia, alikuwa wa kawaida na kuongeza hiyo ndiyo sababu ya familia kushtuka.

“Kwanza alikuwa likizo na ilitakiwa asafiri siku ya Jumamosi, kwa hiyo alitoka siku hiyo kwenda kununua kitu ndipo alipokamatwa, tunaomba Jeshi la Polisi lionyeshe ushirikiano kubaini yupo kituo gani ili tujue ni kosa gani anakabiliwa nalo ili hatua nyingine zifuate,” alisema Magoti Edwin.

Chanzo: mwananchi.co.tz