Siku chache baada ya Serikali kutangaza kuwa kampuni ya Chalinze Cement ilifutwa kwa mujibu wa sheria, wadau wameibuka na kuhoji juu ya kampuni hiyo.
Katika mkutano na waandishi wa Habari, Wakili wa Chalinze Cement, Melchisedeck Lutema akizungumzia kufutwa kwa kampuni hiyo na msimamo wao juu ya kuendelea kupinga muunganiko wa kampuni za Tanga Cement na Twiga Cement amedai hawakupewa nafasi ya kusikilizwa.
Kauli hiyo pia imekuja ikiwa ni siku chache tangu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk Ashatu Kijaji kulieleza Bunge kuwa kampuni ya Chalinze ambayo imekuwa kinara kupinga muunganiko huo, ilifutwa kisheria baada ya kubainika kutoa maelezo ya uongo wakati wa usajili na kushindwa kujieleza ndani ya siku 30 walizopewa.
Kutokana na hatua hiyo baadhi ya wadau wamehoji juu ya jambo hilo..”Kwa muda sasa nimekuwa nikifuatilia kampuni inayojiita Chalinze Cement na nilichokiona kinachekesha. Je, unajua kwamba kampuni hii haimiliki ardhi yoyote ambayo inaweza kuchimba mawe ya chokaa kwaajili ya uzalishaji wa simenti? Pia haina hata chapa wanayodai kuwa nayo. Hawaingizi hata sementi nchini kupitia bandari zetu zozote za Tanzania,”.