Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Safari ya huzuni kijijini Lupaso

2c0551e779c0c72eeececaff35158230 Safari ya huzuni kijijini Lupaso

Tue, 28 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SAFARI ya kikazi niliyoianza na wafanyakazi wenzangu watatu kutoka jijini Dar es Salaam kuelekea kijijini Lupaso, wilayani Masasi, mkoani Mtwara kwa ajili ya mazishi ya Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, ilikuwa ya simanzi na huzuni.

Huzuni ilijidhihirisha hata katika vijiji, miji na maeneo yaliyozoeleka kuwa na uchangamfu mkubwa unaochagizwa na shughuli za kibiashara.

Ingawa safarini tulijaribu kuzungumza habari nyingine, lakini zote ziliishia kumwelezea Rais mstaafu Mkapa namna alivyopigania uchumi wa Tanzania na kuiweka nchi kwenye ramani ya dunia kiuchumi. Tuliishia kusema Mzee Mkapa ameacha alama kubwa kwa vizazi na vizazi.

Hali ya hewa ilizungumza, miti, mingi ikiwa mikorosho ilijizuia kujipeperusha kwa furaha yake ya asili, bila shaka hata wadudu, wanyama na viumbe vingine, vilihisi hali ya tofauti kutokana na kifo cha Rais mstaafu Mkapa, mtu mwenye sifa njema nyingi kuliko mbaya, mzee wa uwazi na ukweli, Big Ben au wengine wakimwita Mr Clean.

Askari wa zamu barabarani nao walionekana kupunguza ukali wa kuhoji makosa na uhakiki wa magari, pamoja na kwamba sauti zao walipotusimamisha mara kadhaa barabarani zilizoonekana zenye ukakamavu wa kijeshi, mioyo yao ilijawa na machozi pale walipogundua kwa siku chache zilizopita, idadi kubwa ya wasafiri wanaoelekea kusini mwa nchi, wanakwenda katika mazishi ya Rais mstaafu Mkapa.

Binafsi nilidhani utulivu huu ni kwa maeneo machache njiani, kumbe sivyo, mazingira yaliyozoeleka kuwa na shamrashamra na shughuli nyingi za kibiashara na kijamii, Wilaya ya Masasi, ilikuwa kimya isivyo kawaida.

Juzi baadhi ya watu walikuwa wakifuatilia katika luninga zao ibada na shughuli kutoa heshima za mwisho na kumuaga kipenzi cha wengi, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa katika Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam. Hata jana walikuwa wakifuatilia pia.

Vijana wa bodaboda hapa Masasi walizungumza kwa huzuni. Walieleza kuumizwa kwa kifo cha Mkapa ambaye kwao wengi ni babu na baba kwa wachache wao.

“Sisi huku kusini kwa kweli tumekumbukwa sana kimaendeleo kwa sababu ya Mkapa. Hata sisi pamoja na kwamba tunafanya biashara kwa uhuru kutokana na Rais wetu wa sasa Magufuli (Dk John) kutukingia kifua, lakini ukweli tumepiganiwa sana na Rais Mkapa enzi alipokuwa madarakani,” anasema Zacharia John, dereva wa bodaboda Masasi Mjini.

Vijana hao wa bodaboda kwa nyakati tofauti pamoja na kupata wageni wengi wanaohitaji huduma yao ya usafiri, wanakiri mioyo yao imejaa uchungu na huzuni kubwa.

Masasi ni mji wa biashara, lakini uchangamfu wa kibiashara uliozoeleka, umepungua na inaelezwa na wakazi kwamba hali hiyo ilikuja mara tu baada ya Rais Magufuli kutangaza msiba huo mzito uliolipata taifa.

Rais Mkapa amekuwa msuluhisi wa migogoro katika nchi mbalimbali za Afrika ikiwamo Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Ulezi, utu wema na busara zake pia zitaendelea kukumbukwa kote duniani.

Barabara yenye urefu wa kilometa 11 aliyozawadiwa na Rais John Magufuli mwaka jana, ambayo ni maungio ya barabara ya kuelekea Newala ya urefu wa zaidi ya kilometa 30 ndio atakayopitishwa kesho.

Alizoea kupita akiwa mzima sasa atapita akiwa kwenye jeneza, akiwa hana uwezo kuwapungia na kuwasalimia wananchi aliyozoea kuwasalimia alipokuwa akipita kila Krismasi au Pasaka, alipokuja kijijini Lupaso lakini sasa wao ndio watakuwa wanampungia mkono wa kumwaga.

Kazi ya kupunguza matawi ya miti yaliyozidi na kufunika sehemu ya barabara inaendelea kijijini hapa. Wananchi wapo bega kwa bega na serikali kwa maandalizi haya ya kihistoria.

Diwani wa Kata ya Lupaso, Douglas Mkapa, ambaye ni mtoto wa kaka wa marehemu, anasema wananchi wamejitokeza kwa wingi kumuandalia baba yao sehemu atakayolala daima akisubiri ufufuo (kulingana na imani ya dini nyingi).

Kaburi linachimbwa na kujengwa kwa ustadi mkubwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) baada ya juzi Jumamosi, kiongozi wa ukoo, Chifu Mkonona kuwaonesha mahali ambapo mwenyewe alielekeza akifa, azikwe. Sehemu hiyo ni pembeni kabisa mwa kaburi la baba yake, Mzee William Matwani.

Majirani, familia na uongozi wa wilaya kwa usimamizi wa karibu wa Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Selemani Mzee, wanaendelea na maandalizi. Matingatinga yamesafisha na kusawazisha kwenye vilima nyumbani kwa Mkapa ili waombolezaji waweze kukaa vizuri japo kwa huzuni na simanzi kubwa.

Mazingira ya nyumbani kwa Mkapa yamegubikwa na huzuni yenye matumaini makubwa kwamba hapo alipo, amelala pema. Hii ni kwa sababu ya sifa yake kubwa kijijini ya upendo na ucha Mungu wake. Makundi ya watu wanahakikisha pia kuna huduma za afya na maji ya kunawa mikono kwa sabuni kila kona ikiwa ni hatua ya kupambana na virusi vya corona.

Kudhihirisha kuwa ni mcha Mungu, pembeni, upande wa kulia wa mlango mkubwa wa pembeni ukiwa unaingia ndani ya nyumba yake, Oktoba 16, mwaka 2004 Mkapa mwenyewe aliweka jiwe la msingi lenye maneno ya Biblia katika sentensi mbili zifuatazo; ya kwanza inasema “Bwana asipoijenga nyumba, waijengayo wanafanya kazi bure” na ya pili inasema “Bwana asipoulinda mji, yeye aulindae akesha bure” akinukuu Zaburi ya 127:1-2.

Kanisa Katoliki, alikozaliwa na kulelewa baba yake akiwa katekista katika parokia ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu kijijini hapo, linatambua ucha Mungu wa Mkapa na kwa taarifa za Paroko wa parokia hiyo, Padri Jude Massawe, Misa Takatifu ya maziko inatarajiwa kuongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Songea, Damian Dallu.

Askofu wa Jimbo la Tunduru-Masasi, Filbert Mhasi, pia atashiriki ibada hiyo huku maaskofu, mapadri, watawa na watu wa imani mbalimbali wanatarajiwa kuhudhuria maziko hayo.

Msemaji wa msikiti wa kijiji hicho alioujenga Mkapa, Mohamed Kitambi anasema taa imezimika, Mkapa amelala na hatoamka tena, lakini wema wake usio na ubaguzi wa kidini, kikabila wala rangi, utaendelea kuishi vizazi hata vizazi.

Safari ya mwisho hapa duniani ya Rais mstaafu Mkapa, aliyezaliwa kijijini Lupaso mwaka 1938 akiwa mtoto wa mwisho wa mzee Matwani na yeye kupewa jina la Mkapa la ujombani kwa mujibu wa Wamakua, ilifika usiku wa Alhamisi, Julai 23 mwaka huu kuamkia Ijumaa hospitalini, jijini Dar es Salaam. Taifa lilitangaziwa msiba huu mzito na Rais John Magufuli kwa huzuni kubwa.

Masasi imenyamaza, Lupaso inalia, Mtwara inahuzunika, Watanzania tunalia. Tangulia mpendwa wetu Benjamin William Mkapa, shujaa na jasiri wa daima.

Chanzo: habarileo.co.tz