Hai. Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya amewaweka ndani viongozi wa Chama cha Ushirika Narumu Manushi kwa madai ya kuwadhulumu wananchi wa vijiji vinne kupata haki zao katika shamba la Fofo lenye ukubwa wa ekari 106.
Pia, ametoa siku saba kwa wananchi waliojenga nyumba katika shamba hilo kubomoa kabla hatua za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao.
Sabzya ametoa amri hiyo leo Alhamisi Septemba 12, 2019 na kubainisha kuwa kwa sasa shamba hilo ni mali ya Serikali na si kikundi cha watu 46, wanaojiita wanachama wa ushirika Narumu Manushi.
Amesema shamba hilo limekuwa na mgogoro kwa zaidi ya miaka 50, kwa sasa litakuwa linamilikiwa na vijiji vinne vya Urori, Tela, Mlama na Usari vilivyopo kata ya Machame Narumu.
Ofisa ardhi wilaya ya Hai, Jacob Mghumba amesema shamba la Fofo mmiliki wake wa awali alikuwa Dk Phones Fofo na baadaye umiliki ukarudi serikalini.
Filbert Kiondo, katibu wa ushirika huo amesema shamba hilo walilipata baada ya kulipa deni la Sh100,000.