Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sababu za wananchi wilayani Tanganyika kukimbia urasimishaji ardhi zabainishwa

Ardhi Pic Sababu za wananchi wilayani Tanganyika kukimbia urasimishaji ardhi zabainishwa

Wed, 19 Jul 2023 Chanzo: Mwananchi

Uelewa mdogo kuhusu umuhimu wa kurasimisha ardhi kwa ajili ya kupata hati za kimila, ni moja ya sababu iliyosababisha baadhi ya wananchi wa kijiji cha vikonge wilayani Tanganyika, kuwakimbia wapimaji wakihofia kuporwa ardhi yao.

Wakizungumza na Mwananchi Digital kijijini hapo jana, baadhi ya wananchi hao Nzige Lushinge ambaye ni mkazi wa Kitongoji cha Mnyamasi B, amesema Serikali ilipoanza kurasimisha ardhi katika eneo hilo, wengi hawakufahamu manufaa yake.

“Viongozi walitupa elimu lakini wengine walikuwa wagumu kuelewa umuhimu wake, wakati zoezi la upimaji likiendelea wapo waliokimbia na kujificha ili kuwakwepa wapimaji, wakidhani wamekuja kupora maeneo yao,” amesema na kuongeza;

“…ni uelewa mdogo…walidanganyika, si unajua ukiambiwa jambo tena linahusu kuchukuliwa kwa ardhi yako, na kumbuka huuu ndiyo uridhi wako kwa vizazi vyako, sasa ukiambiwa kuwa kuna watu wanataka kuchukua mali hiyo, utatafuta mbinu ya kuilinda. Sasa wenzetu waliamua kuwakimbia wapimaji.”

Kwa mujibu wa Lushinge, watu waliambiwa kuwa Serikali kwa kushirikiana na taasisi ya Jane Goodall, wanampango wa kuchukua maeneo yao kwa njia ya kuwahadaa wakitumia upatikanaji hati za kimila baada ya kupimwa kwa maeneo yao.

Aidha amesema waliojitokeza kupimiwa maeneo yao wamepata faida baada ya kupata hati hizo ambazo zinawawezesha kuwa wamiliki wa ardhi kisheria lakini pia kutumia hati hizo kuomba kupata mikopo katika taasisi za kifedha.

“Nikuambie mwandishi, hofu ilianza kutokana na ukweli kuwa, watu wengi wamepata maeneo waliyonayo bila kuyanunu, hii inatoka na ukweli kuwa maeneo mengi huku yalikuwa mapori, watu walijichukulia tu, hivyo waliogopa Serikali isije kutumia mbinu ya kuyapima, kumbe ndiyo inayachukua,” amesema.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Vikonge, Steven Msome; amesema kijiji hicho kina zaidi ya kaya 2000, hata hivyo ni kaya 1800 ndizo zilijitokeza katika zoezi zima la upimaji na kwamba kwa awamu ya kwanza, hati miliki 800 zimetolewa kwa wanakijiji hao.

Msome kwa upande mwingine anauona mpango huo kama suluhisho la migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji ambao wanadaiwa kukatana mapanga na kusababisha vifo.

“Niwashauri wananchi wangu kwa kuwa wameona manufaa sasa wabadilike, mipaka ya hifadhi na maeneo ya malisho ya mifugo sasa imetambulika, atakayevamia maeneo hayo anatafuta kesi kwa nguvu na sheria itachukua mkondo wake,” amesema.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geofrey Pinda; ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, amewasisitiza wananchi kuendelea kurasimisha maeneo yao.

“Naomba mtunze hati mlizopata, tumejenga ofisi hapa nyumbani kama kuna shida tuanzie ofisini, zoezi ni endelevu endeleeni kujitokeza kupimiwa achaneni na imani potofu,” amesema Pinda.

Akizungumza kwa niaba ya taasisi ya Jane Goodall Tanzania, mratibu wa mradi wa Landscape Conservation in Western Tanzania (LCWT) Dk Kasukura Nyamaka amesema mradi huo unatekelezwa katika vijiji 104 katika mikoa ya Katavi na Kigoma.

Chanzo: Mwananchi