Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sababu za kunenepesha mbuzi wako

48213 Pic+mbuzi

Sat, 23 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Unenepeshaji wa mbuzi ni hatua ambayo mbuzi hutengwa na kuwekwa katika eneo moja kisha kulishwa vyakula vya protini na nguvu kwa wingi kwa lengo la kupata nyama nyingi, safi na bora pamoja na soko la uhakika.

Hatua hii inayofanywa na mfugaji kabla ya kuuza mbuzi wake, huchukua takribani miezi miwili mpaka minne kabla ya kuchinja ama kuuza mbuzi wake.

Sababu ya kunenepesha mbuzi

Tunanenepesha mbuzi kwa lengo kubwa la kuongeza ubora wa nyama (upatikanaji wa nyama nyingi zenye viwango) hasa kwa viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa pamoja na kupata nyama laini na yenye ladha.

Pia, tunanenepesha ili kufanya uzalishaji wa nyama kibiashara ili kukidhi mahitaji ya nyama na kuongeza kipato kwa mfugaji.

Mbuzi karibu wote wanafaa katika kunenepesha, kikubwa tu ni kuhakikisha unafuata taratibu za unenepeshaji ikiwa ni pamoja na kulenga kupata nyama na si kulisha mbuzi kupata maziwa na nyama kwa wakati mmoja. Mbuzi wa kienyeji na mbuzi chotara wanafaa kunenepesha. Ni vizuri zaidi kunenepesha madume na kuzingatia kutoruhusu kupanda mbuzi jike.

Mbuzi jike anaweza kunenepeshwa pia kwa kutompandisha tena baada ya kuacha kunyonyesha na kukausha maziwa ambapo atakuwa akilishwa kwa ajili ya kupata nyama tu.

Chakula cha kunenepeshea mbuzi

Katika unenepeshaji wa mbuzi, vyakula vya kwenye makundi mawili makuu yaani protini na vyakula vya kutia nguvu vinahitajika kwa wingi sana.

Vyakula vya protini: Vyakula hivi ni pamoja na mbegu za pamba, soya, mbegu za alizeti, majani ya kaliandra, sesbania, nyasi, majani ya mahindi machanga, majani ya viazi vitamu, majani ya maharagwe, majani ya njegere, desmodium, na lusina.

Vyakula vya kutia nguvu: Vyakula vya kutia nguvu ni pamoja na matete, ukoka, majani ya tembo, seteria na Guatemala. Vyakula vya kutia nguvu pia vinaweza kutokana na aina zote za nafaka, punje za ngano, au molasesi.

Maji: Maji yanatakiwa yapatikane saa zote na yawe safi, salama na ya kutosha.

Cha kuzingatia wakati wa unenepeshaji wa mbuzi

Mbuzi wanaonenepeshwa wanahitaji maandalizi mazuri na madhubuti ikiwamo kukinga magonjwa, kutibu, kutoa dawa za minyoo, kupata eneo kwa ajili ya kunenepeshea na upatikanaji wa chakula na maji.

Katika unenepeshaji wa mbuzi, kuna baadhi ya vitu vya kuzingatia ikiwamo upatikanaji wa banda. Mbuzi ni lazima watengenezewe ama wajengewe banda imara na la kuwatosha kwa ajili ya kunenepesha kwani mbuzi watakuwa sasa wanalishwa kwa mfumo wa ndani.

Ukaguzi wa kina kwa mbuzi mmoja mmoja ufanyike ili kubaini afya yake na kuzuia hasara inayotokana na vifo. Ikiwezekana nyunyizia dawa ya kinga na kuua wadudu wasumbufu. Hakikisha mbuzi unaowatenga kwa ajili ya kunenepesha hawana magonjwa na pia wamepata chanjo ya kutosha kuwakinga na magonjwa.

Kabla hujaamua kufanya mradi wa kunenepesha mbuzi, hakikisha una uwezo wa kupata lishe sahihi na kamili kwa ajili ya mbuzi wako. Hii ni kwa sababu kama kutakuwepo na uhaba wa lishe kwa muda wa kunenepesha, hutoweza kufikia malengo badala yake mbuzi watabaki vilevile na huenda wakadhoofika kuliko walivyokuwa awali.

Hakikisha katika eneo lako la unenepeshaji kunakuwapo maji ya kutosha, safi na salama. Hii ni kwa sababu mbuzi watahitaji kunywa maji sana na kwa wakati wote banda lazima liwe na maji.

Katika kuweka uwiano wa chakula na maji, angalau kwa kila kilo moja ya chakula iende na maji lita nne. Wakati wa unenepeshaji, mbuzi wanatakiwa wawe bandani na waletewe chakula ndani ya banda na si kuwaachia tena kwenda kutafuta malisho.

Kumbuka kuwa mbuzi waliokuwa wameachiwa kujilisha wenyewe wamezoea kujipatia aina mbalimbali ya majani na wanayoyapenda wenyewe hivyo ni vyema pia kuhakikisha wanapatiwa vyakula hivyo hata kama si vyote kwa wakati mmoja.

Makala kwa hisani ya mkulima mbunifu. www. mkulimambunifu.org



Chanzo: mwananchi.co.tz