Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sababu za kuachiwa kwa anayedaiwa kumuua jirani kwa kisu

Jirani Kisuuuu Sababu za kuachiwa kwa anayedaiwa kumuua jirani kwa kisu

Sun, 26 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkazi wa Mbweni, Boi Rajabu (65) ameachiwa huru baada ya kushinda kesi ya mauaji aliyotuhumiwa kumuua jirani yake kwa kumchoma kisu.

Katika kesi hiyo, mshtakiwa huyo alidaiwa Februari 8, 2019 eneo la Mbweni Miti mitatu, Wilaya ya Kinondoni alimuua Abas Mwinjuma kwa kumchoma kisu tumboni na mgongoni hadi utumbo kutoka nje.

Mpaka anaachiwa huru juzi na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mshtakiwa huyo alikuwa ameshakaa gerezani miaka minne.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Romuli Mbuya alisema mshtakiwa alihusishwa na kifo cha Abasi kwa kutajwa na mtu mmoja aliyeitwa Adam Matutu ambaye hata hivyo hakupelekwa mahakamani kutoa ushahidi.

“Matutu ndio mtu pekee aliyewataarifu watu wote wa eneo hilo kuwa aliyemchoma kisu ni Boi, sasa bila ushahidi wa mtu huyo mahakama haiwezi kuthibitisha mashtaka dhidi ya mshtakiwa.

“Huyo Matutu ndio angetuambia hizi habari za Boi kumchoma kisu Abas alizitoa wapi? Alishuhidia tukio au aliambiwa na marehemu,” alisema

Hakimu huyo alisema ushahidi pekee unaomuunganisha mshtakiwa na tuhuma hizo ni wa shahidi wa sita, Koplo Erasto kutoka kituo cha Polisi Mbweni aliyeandika maelezo ya onyo ya mshtakiwa na katika mahojiano na mshtakiwa alikiri kumuua Abas kwa kumchoma kisu.

Hata hivyo, alisema ushahidi wa Koplo Erasto haukuwa na nguvu kwa kuwa mshtakiwa alikana maelezo yake akidai alilazimishwa kusaini maelezo ambayo hakuyaandika.

Hivyo, Hakimu Mbuya alisema hakuna ushahidi wa moja kwa moja uliungwa mkono na mashahidi kuoyesha jinsi mshtakiwa alivyomchoma kisu mlalamikaji.

“Mahakama imeridhika kuwa kosa linalomkabili mshtakiwa, upande wa mashtaka wameshindwa kuthibitisha shtaka dhidi yake, hivyo Boi unakuachia huru kuanzia sasa” alisema Hakimu Mbuya.

Baada ya Hakimu Mbuya kutamka kumwachia huru mshtakiwa hiyo aliendelea kusimama kizimbani hadi wakili wake, Hilda Mushi na Gerson Mosha walipomwambia, “mzee umeachiwa huru na mahakama.”

Hata baada ya kuelezwa hayo alionekana kuendelea kushangaa kwa muda na baadae machozi yalianza kumtiririka.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live