SABABU ya mauaji ya Mwenyekiti wa Kitongoji cha Urua Chini wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro, Augustine Moshi (35) aliyejinyonga baada ya kumuua kikatili mkewe kwa kumchija shingo, zimetajwa kuwa ni ugomvi wa muda mrefu wa wanandoa hao uliohusisha faragha ya tendo la ndoa.
Kwa mujibu wa viongoozi wa Kijiji cha Mfuruashe pamoja na baba wa Augustine, wanandoa hao wamekuwa na mgogoro wa muda mrefu ambao uliwafikisha hadi katika Jeshi la Polisi, viongozi wa dini na kwa familia zao.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mfuruashe, Kata ya Mengeni Chini wilayani Rombo, Elipidi Shao alisema wanawanandoa hao wamekuwa na ugomvi wa mara kwa mara ambao ni sugu.
Alisema uongozi wa Serikali ya Kijiji umeshiriki katika kusuluhisha ugomvi wa wanandoa hao ambapo mke wa Augustine, alikuwa akimlalamikia mumewe kuwa na tabia mbaya wakati wa faragha ya tendo la ndoa.
Alisema mbali na uongozi wa kijiji kujitahidi kusuluhisha wanandoa hao, pia wamesuluhishwa mara nyingi na uongozi wa kanisa, Dawati la Jinsia la Polisi wilayani humo na familia bila mafanikio.
“Mke analalamika mumewe sio mwaminifu, ana michepuko, ana anapenda kumtendea vibaya, na juzi walipelekana polisi ikashindikana wakasema warudi kijijini wasuluhishwe na viongozi wa vijiji na tulishirikiana na jumuiya na tukawapatanisha. Sasa sijui nini kiliwapata hadi kufanya maamuzi hayo,” alieleza mwenyekiti huyo wa kijiji.
Baba mzazi wa Agustine Moshi ambaye alikuwa mshereheshaji (MC), Audifas Moshi, alisema mwanawe alikuwa na ugomvi wa muda mrefu na mkewe wa masuala ya unyumba katika ndoa yao.
“Walikuwa na ugomvi wa muda mrefu wa masuala ya unyumba na masuala ya unyumba unajua yana ufafanuzi wake. Ila mke wake alikuwa akimsingizia kwamba anamtendea vibaya, jambo ambalo lilimletea msongo wa mawazo,” alisema baba wa mume huyo.
Alisema mwanawe huyo mbali na kuwa na msongo wa mawazo, pia alikuwa na ugomvi na mkewe baada ya kutaka kuuza duka alilomfungulia kwa ajili ya kulipa madeni aliyokuwa nayo.
“Mke wake aliugua na alimtibu kumbe pesa alikuwa anakopa baada ya mke kupona akamuomba auze hilo duka warudishe madeni ya watu mke akawa anakataa akiona atafilisika ndo ugomvi...ambao tuliusuluhisha tarehe nane kabla ya vifo vyao usiku wa kuamkia tarehe tisa mwezi huu,” aliongeza baba huyo.
Wanandoa hao wameacha watoto watatu ambao ni Audifas Agustine (12), Adeline Agustine (8) na Maria Agustine (6) na kwamba mazishi yanatarajiwa kufanyika kesho kijijini kwao.
Augustine alimuua mkewe Anastasia Augustine (31) kwa kumkatakata na kitu chenye ncha kali na kisha kujiua kwa kujinyonga na waya kwa kile kinachodaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi.
Mauaji hayo yalifanyika katika Kijiji cha Mfuruashe Kata ya Mengeni Chini usiku wa Novemba 8, mwaka huu.