Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sababu hekari mbili za mahindi kufyekwa Mpanda

EDC0C142 F7DD 407D B090 01FABFADCD4C.jpeg Sababu hekari mbili za mahindi kufyekwa Mpanda

Sat, 16 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Dar es Salaam. Kufuatia shamba la mahindi zaidi ya hekari mbili kufyekwa wilayani Mpanda Mkoa wa Katavi, Mkuu wa wilaya hiyo, Jamila Yusuph amesema mahindi hayo yalipandwa kinyume cha sheria.

Amesema kulingana na sheria ndogo za manispaa hiyo, hakuna mwananchi anayeruhusiwa kupanda mazao yanayovuka urefu wa goti katikati ya mji kwani ni kuhatarisha usalama wa raia na mali zao.

Kwa mujibu wa Sheria ya mipango miji ya halmashauri hiyo namba 355, chini ya kanuni kifungu 77(1)(r) namba (5) hakuna mtu anayeruhusiwa kufanya shughuli za kilimo katika maeneo yaliyotengwa kuwa sehemu ya miji.

Licha ya sheria kukataza hivyo, mkulima ambaye mahindi yake yamefyekwa, amerudia kosa alilotenda mwaka jana na kusamehewa, huku akitakiwa kulipa faini lakini mwaka huu tena amerudia kosa hilo.

Akisikiliza kero za wananchi na wafanyabishara wa Soko la Mpanda Hotel jana Ijumaa, Desemba 15, 2023 mkoani Katavi, mkuu huyo wa wilaya aliwataka wananchi kuzingatia sheria.

“Watendaji wachukue hatua haraka iwezekanavyo kabla mazao hayajawa marefu ili kutosababisha kuwagombanisha wananchi na Serikali yao,” amesema DC huyo kupitia taarifa yake kwa umma iliyotolewa na mkurugenzi wa halmashauri.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, Sophia Kumbuli amewataka watendaji wa kata kuendelea kuwakumbusha wananchi kutii sheria bila shuruti.

Amesema ili kuimarisha usalama wa wilaya, walitunga sheria ndogo kuwataka wananchi kutopanda mazao yanayovuka magoti kwani vichaka ndivyo vinatumika na wahalifu kutenda unyama kwa raia.

“Sasa huyu mkulima alilima mwaka jana akakamatwa akapigwa faini na akakiri kosa na kusainishwa kuwa hatorudia, mwaka huu akapanda tena akaitwa akahojiwa, lakini wananchi wamekuwa wakilalamika kwa nini yeye hatii,” amesema.

Sophia amesema licha ya mkulima huyo kupelekwa hadi baraza la kata alijinadi atalipa faini na maisha yaendelea jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Amesema ndani ya manispaa hiyo, wameonyesha ni maeneo gani watu wanapaswa kulima, lakini katikati ya miji ni marufuku kupanda mazao yanayovuka magoti.

Jitihada za kumpata mkulima huyo zinaendelelea.

Kupitia mtandao wa kijamii wa X muda mfupi baada ya picha ya tukio hilo kupakiwa kwenye mtandao huo, mwananchi anayetambulika kwa jina la mkulima wa Katavi aliandika,

“Kuna mambo hufanyika ili baadaye ilaumiwe Serikali, Mpanda mjini inajulikana mazao marefu hayaruhusiwi kulimwa isipokua mazao mafupi, ni utaratibu wa miaka sasa kila mtu anajua, na kila masika mkurugenzi hutoa matangazo, lakini bado wanalima, asilaumiwe mtu hapo walitangaza.”

Naye Adrew Principle kupitia mtandao huo, amehoji kwa nini mamlaka husika isingeacha mahindi yakomae ndipo watoe onyo.

“Je hapakuwa na meza ya majadiliano hadi kufanya unyama huo? na kwa nini kamati ya ulinzi ikaruhusu haya,” amehoji.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live