Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sababu Mtwara kuporomoka mikoa iliyofanya vyema kidato cha sita hii hapa

Wed, 17 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mtwara. Mkuu wa Mkoa wa Mtwara,  Gelasius Byakanwa  amesema  mkoa huo umeshika nafasi ya tatu kitaifa katika matokeo ya mtihani wa kidato cha sita mwaka 2019 kati ya mikoa 29 kutokana na wanafunzi waliofukuzwa kurejeshwa shuleni kufanya mitihani.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatano Julai 17, 2019 katika kikao cha kamati ya ushauri cha mkoa (RCC).

Amesema katika matokeo hayo wanafunzi sita wamepata daraja sifuri, watano walikuwa wamefukuzwa shule lakini waliruhusiwa kufanya mtihani.

 “Nafasi yetu imeshuka kwa nafasi mbili lakini ni kwa sababu tumekuwa na sifuri sita, tunajua sababu za kushuka. Shule ya Chidya wanafunzi walifanya vurugu wakafukuzwa na kati ya waliofukuzwa wanne wamepata sifuri.”

“Mwanafunzi aliyepata sifuri shule ya Akwinasi naye alikuwa mpenda vurugu alifukuzwa mpaka kipindi cha mitihani kwa hiyo tulikuwa tunajua hao watatusababishia sifuri,” amesema mkuu huyo wa Mkoa.

Amefafanua kati ya wanafunzi 1,970  waliopata daraja la kwanza ni 453, daraja la pili ni 949, daraja la tatu 544 , daraja la nne ni 18 na daraja sifuri ni sita.

Pia Soma

“Ni kazi kubwa kipekee mfano tuna shule ya Serikali ya Ndanda  ilikuwa na wanafunzi 477 kati yao wawili tu ndio wamepata daraja la nne, wanafunzi 102 wana ufaulu wa daraja la kwanza, 231 wana daraja la pili, 142 wana daraja la tatu,” amesema Byakanwa

Waliopata sifuri

Septemba 2,2018 baadhi ya wanafunzi wa shule ya wavulana ya Chidya walifanya mgomo pamoja na kuharibu mali zenye thamani ya Sh18 milioni .

Wanafunzi hao walidaiwa kuvamia nyumba ya mkuu wa shule, mwalimu wa taaluma na mwalimu wa malazi  na kisha kuharibu mali za ndani na kuchoma  pikipiki mbili moja ikiwa mali ya shule na nyingine ya mwalimu.

Baada ya uchunguzi wanafunzi 23 kati ya 282 waliohusika na vurugu walikutwa na hatia na kisha bodi ya shule kukaa na kuwafukuza, kati yao wapo ambao matokeo yao yametangazwa hivi karibuni.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz