Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

SMS yadaiwa kusababisha mume kuua mke

SMS Mauaji SMS yadaiwa kusababisha mume kuua mke

Fri, 5 Apr 2024 Chanzo: Mwananchi

Mwanamume mkazi wa Mtaa wa Umoja, Mji Mdogo wa Bomang'ombe, wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro anadaiwa kumuua mkewe, Mariam Johnson kwa madai ya kumkuta na ujumbe wa maneno (SMS) unaodaiwa kuwa wa mapenzi kutoka kwa mwanamume mwingine.

Inadaiwa baada ya mwanamume huyo kutekeleza mauaji aliacha ujumbe wa maandishi kitandani ukieleza sababu ya kumuua mkewe ni kwamba, uvumilivu umemshinda kutokana na usaliti wake na kisha kumfungia ndani na kutokomea kusikojulikana.

Baada ya tukio hilo inadaiwa alimtelekeza mtoto wao mwenye umri wa miaka mitatu kwa jirani.

Mauaji hayo yamebainika baada ya mpangaji mwenzake kuhisi harufu kali ikitoka ndani ya chumba walichokuwa wamepanga, huku mlango ukiwa umefungwa kwa nje.

Kutokana na hali hiyo, mpangaji huyo alimtafuta mjumbe wa eneo hilo, Monica Musin na kumpata taarifa ili afike waweze kubaini ni harufu ya kitu gani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema tukio hilo lilitokea April 3, 2024 na kwamba wanamsaka mwanamume aliyehusika na mauaji hayo.

Gari la polisi lenye mwili wa mwanamke huyo likiwa nje ya nyumba alikokutwa marehemu. Picha na Janeth Joseph

"Huyu ni mtu ambaye alikuwa na mume wake lakini changamoto inayoonekana ni wivu wa mapenzi, kwa sababu huyu bwana alikuwa akimtuhumu mke wake kwamba alikuta meseji (sms) ya mwanamume mwingine kwenye simu ya mke wake, inaonyesha shida ndipo ilipoanzia," amesema Kamanda Maigwa

"Mwanamume ni kama alimziba pumzi, maana majirani walikuwa wakisikia ugomvi ndani wakati huo wa usiku, baada ya mwanamume kuchukua maamuzi hayo ameacha ujumbe kwamba ameamua kuchukua uamuzi huo kutokana na kitendo cha mke wake ambaye alikuwa akimwamini, alimsaliti," amesema.

“Kwa hiyo hakuna ubishi kwamba ni yeye aliyetenda kile kitendo, tunamtafuta kwa kuwa mwanamume aliacha ujumbe wa kuthibitisha kwamba yeye ndiye aliyetenda kitendo hicho kwa sababu ya wivu wa mapenzi," amesema Kamanda Maigwa.

Awali, akizungumzia tukio hilo, Mjumbe wa eneo hilo, Monica Musin amesema baada ya kupata taarifa kwa mmoja wa wapangaji alifika hapo na kutokana na hali iliyokuwapo alimtafuta mwenyekiti wa kijiji kwa ajili ya kutafuta utaratibu wa kuvunja mlango ili kuona ni nini kipo ndani.

Amesema, "wakati tunakuja eneo la tukio na mwenyekiti niliambatana na mume wangu. Mwenyekiti yuko nyuma, mume wangu akawa anamhoji mpangaji aliyetoa taarifa, akamuuliza nini kimetokea akamwambia usiku alisikia kelele kubwa, baada ya muda kidogo kukawa kimya, baadaye akawa anasikia mtu anatoka mara anaingia kwenye hicho chumba," amedai.

Amedai, "kwa sababu ni kawaida yao kupigana wakajua hawa washapigana na kwamba, hakuna aliyeshtuka kuwa kuna mauaji. Kwa maneno hayo mume wangu akawa na wasiwasi kama kuna kitu kimetokea, ikabidi apige simu polisi. Askari walikuja wakaingia ndani wakakuta hali ndiyo hivyo."

Amedai kwa mara kadhaa amekuwa akipokea taarifa za ugomvi wa wawili hao na kwamba, walikuwa wakipigana na ilifika mahali waliachana kabla ya kurudiana na ndipo mauaji yalipotokea.

"Nimeshapokea malalamiko mengi na si mara moja, wamekuwa wakigombana na kupigana mpaka walishafikishana kwenye dawati la jinsia, na ilifika mahali waligombana kabisa na kuachana. Sasa juzijuzi tu tumeona wamerudiana," amedai.

Mwenyekiti wa mtaa huo, Godfrey Maimu amesema, "tulipiga simu polisi kuomba ushirikiano, askari walipofika walivunja mlango tukangia ndani tukakuta mwili uko pembeni mwa kitanda na ulikuwa umevimba sana."

"Tulikuta ujumbe umeandikwa kwenye karatasi, hatukuusoma, japo tulikuwa na shauku kubwa kujua ni nini ambacho kimeandikwa, askari walipiga picha na kuondoka na karatasi," amesema.

Chanzo: Mwananchi