Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

SIMCU yatenga Mil. 36 kusaidia shughuli ya kijamii

Walemavuu.webp SIMCU yatenga Mil. 36 kusaidia shughuli ya kijamii

Thu, 4 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chama kikuu cha Ushirika Mkoani Simiyu(SIMCU) kimetenga fedha kiasi cha Sh mil 36.7 katika msimu wa pamba 2019/2020 kwa ajili ya kutekeleza shughuli za kijamii na kurudisha shukrani kwa wananchi.

Kati ya kiasi hicho cha fedha Sh 700,000 zimetumika kumsaidia mtoto Ritha Elias ambaye ni mlemavu wa miguu ili zimsaidie kutatua changamoto ya usafiri na mahitaji yake ya msingi ya shule.

Akitoa taarifa fupi ya utekelezaji wa chama hicho leo wakati wa kumkabidhi mtoto huyo baiskeli ya walemavu kwa ajili ya kutembelea ,kaimu mwenyekiti wa SIMCU, Emmanuel Elias, amesema wameguswa kusaidia jamii katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowazunguka.

Aidha amesema kati ya kiasi hicho kimegusa sekta ya elimu,jamii na afya ambapo Tsh mil 24 zimetengwa kwa ajili ya kusaidia elimu na Mil 12 kwa ajili ya ununuzi wa mashuka katika hospitali zote za Mkoa wa Simiyu.

Awali akikabidhi baiskeli hiyo yenye thamani ya 400,000 kwa mtoto huyo pamoja na fedha taslim sh 300,000 ,Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, amesema chama hicho kimefanya jambo kubwa sana na kutambua umuhimu wa kusaidia wenye uhitaji.

"Sio siri chama cha SIMCU Simiyu mmefanya jambo kubwa na la maana ambalo litaenda kuacha historia kwa vizazi na vizazi...msaada huo mlioutoa utageuka baraka kwa mtoto huyo na chama kwa ujumla,nawapongeza sana na muendelee na moyo huo" amesema Kiswaga.

Nae bibi wa mtoto huyo Ritha Elias, Perpetual Mtaima amekishukuru chama hicho pamoja na uongozi wa Mkoa kwa ushirikiano waliouonesha kwa mjukuu wake.

Amesema ni matumaini yake kwa sasa mjukuu wake atafanya vizuri katika masomo yake kwani hapo awali alikuwa akipata tabu juu ya usafiri.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live