Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

SABA WAKUTWA WAKITEMBEA UCHI BARABARANI

3a9028325a7d9be74c1230b2703962dc.png SABA WAKUTWA WAKITEMBEA UCHI BARABARANI

Sun, 11 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

HALI ya taharuki imewakumba wakazi wa kijiji cha Mvuha, halmashauri ya wilaya ya Morogoro baada ya watu saba kukutwa wakitembea barabarani bila nguo huku tukio hilo likidaiwa kuhusishwa na imani za kishirikina.

Tukio hilo ambalo picha zake zilianza kusambaa katika mitandao ya kijamii linadaiwa kutokea Aprili 7, mwaka huu na baadhi ya mashuhuda walieleza kuwa watu hao wanadaiwa ni wa familia moja na haijajulikana sababu hasa ya kufanya kitendo hicho.

Mmoja wa mashuhuda hao, Mkazi wa Mvuha, Idrisa Kamota aliieleza kuwa siku ya tukio alfajiri wakiwa katika shughuli zao za kawaida walishaangaa kuona kikundi cha watu hao wakiwa katika mstari mmoja bila kuwa na nguo ndipo zikaanza jitihada za kuwazuia wakisaidiana na vyombo vya dola na serikali

“Walikuwa watu saba watoto watatu na watu wazima walikuwa wanne, tulijaribu kuwazuia wasiendelee na safari bila mafanikio hadi wakaja polisi walipowahoji hawakuzungumza chochote ikabidi wawavalishe nguo na kuwaelekeza warudi walipotoka,” alisema Kamota.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mwenyekiti wa kijiji cha Mvuha, Juma Ndunda ambaye pia ni ndugu na familia hiyo, alisema tukio hilo limehusisha familia ya Selemani Mvange akiwa na mke wake, watoto wake wawili na mama yake mkwe pamoja na shemeji zake wawili ambao alikuwa akiishinao nyumba moja.

Alisema taarifa za awali zinaeleza kuwa sababu ya watu hao kufanya hivyo ni madai ya kutaka kurithishwa mikoba ya uganga na kwamba imeelezwa kuna tukio jingine linaweza kutokea katika siku za hivi karibuni ili kutimiza masharti na kwamba suaka hilo limeshafikishwa katika kamati ya ulinzi na usalama wilaya ili kuchukua hatua zaidi.

“Ni kweli tukio hilo limetokea tena, aliyefanya hivyo ni mdogo wangu kabisa sio kwamba hawana akili timamu, ni wazima kabisa ila tulipomuhoji kama familia anadai wanataka kurithishwa mikoba na anasema kuna tukio anataka kufanya, bahati nzuri tumeshafikisha kwa mkuu wa wilaya na alikuja kuzungumza nao,” alisema Ndunda.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Bakari Msulwa aliwataka wananchi wa eneo hilo kuwa watulivu wakati serikali inaendelea kushughulikia suala hilo ambalo linahusishwa na masuala ya kitamaduni.

Alisema baada ya kufanya mazungumzo na familia hiyo aliwachia jukumu la kukutana na kuzungumza na familia husika baada ya kijana huyo kudai hana anachoweza kujibu kwa kuwa alitumwa na wazee kufanya kitendo hicho.

“Kwa sasa hali ni shwari, nilikwenda kuzungumza na familia husika, ili kujua nini kinaendelea kisha nikawaachia kazi wazee wa eneo husika wazungumze na mtoto wao, kwa sababu ni tukio linalohusisha mambo mawili, kwanza utamaduni pia wananchi wanachukulia kama masuala ya kishirikina,” alisema.

Msulwa aliwataka wananchi kuacha kusambaza picha hizo katika mitandao ya kijamii kwa sababu kufanya hivyo ni kinyume na sheria kutokana na picha hizo kutokuwa katika maudhui mazuri.

Chanzo: www.habarileo.co.tz