Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ruwasa washauriwa kuchimba mabwawa ya maji

04189a9a287f80ea72a0335843fd2ddc Ruwasa washauriwa kuchimba mabwawa ya maji

Fri, 12 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wametakiwa kuwa na mkakati wa kuchimba mabwawa katika kila halmashauri ya mkoa wa Dodoma ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa maji.

Wakizungumza katika Mkutano ulioitishwa na Ruwasa chini ya Mkuu Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge jijini hapa, walisema uchimbaji wa mabwawa utakuwa suluhisho la kuondoa kero ya upungufu wa maji katika halmashauri za mkoa huo.

DK Mahenge alisema Ruwasa wanatakiwa kujipanga kuchimba mabwawa katika halmashauri zote nane za mkoa huo kwani kutasaidia kuyatumia kwa shughuli nyingi zikiwemo za kutumia majumbani, kunywesha mifugo na kufanya shughuli za umwagiliaji.

Mkuu wa Mkoa huyo alisema katika kujenga mabwawa ya kupunguza kero ya maji katika halmashauri, Ruwasa inatakiwa kwenda katika halmashauri ili kutoa mwanya kwao kupanga maeneo ya kuchimba kwa ajili ya miradi hiyo ili kufaidisha wananchi wengi zaidi.

Naye Spika wa Bunge wa Bunge, Job Ndugai alisema ujenzi wa mabwawa ni suluhisho la changamoto kubwa ya maji mkoani Dodoma.

Ndugai ambaye ni mbunge wa Kongwa, alisema pamoja na changamoto hiyo bado hali ya maji ni nzuri kutokana na juhudi ya serikali kwani miaka ya nyuma watu walifuata maji kilometa tano na wakati mwingine siku nzima.

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Maduka Kessy alisema Ruwasa wanatakiwa kupanga mipango kuchimba mabwawa ili kusaidia wananchi wengi zaidi katika vijiji vinavyoibuka kuwa miji mkoani humo.

Naye Mbunge wa Mvumi, Livingstone Lusinde alisema Ruwasa imepanga kutekeleza miradi mingi kwa kuweka fedha kidogo, lakini ingetakiwa kutekeleza miradi michache hadi kuikamilisha.

Naye Mbunge wa Kondoa Mjini, Ally Makoa alisema mpango wa mabwawa utasaidia lakini kwa maeneo ya mjini inatakiwa kuchimba visima na usambazaji maji ufanyike majumbani badala ya kuweka vituo vya kuchota ambavyo vinakuwa na mlundikano wa watu huko.

Wakiwasilisha mada, Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Dodoma, Godfrey Mbabaye alisema wakala huo unakisia kutumia takribani Sh bilioni 46.6 katika bajeti ya 2021/2022 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali katika halmashauri nane mkoani Dodoma.

Naye Ofisa wa Ruwasa, Frederick Mageni alisema Ruwasa inatekeleza miradi 167 kati yake 80 ni ya mpango wa malipo kwa matokeo, 25 kutoka kwenye mfuko wa Ruwasa na 62 ni ya wadau mbalimbali wa maendeleo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz