Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ruwasa Kigoma inavyopambana kuhakikisha inamtua ndoo mama

8c2a5b5409f8438f3d4aef56b574a15d.png Ruwasa Kigoma inavyopambana kuhakikisha inamtua ndoo mama

Mon, 10 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

LINUS Robert wa kijiji cha Mabamba, wilayani Kibondo, Kigoma, kwa muda mrefu katika maisha yake anasema wamekuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji. Anasema walikuwa wakitumia muda mrefu kutafuta maji badala ya kufanya shughuli za uzalishaji.

Anasema kuna wakati yeye na wanakijiji wenzake walilazimika kutembea umbali mrefu au kulazimika kununua maji kwa gharama kubwa kwa wauzaji mitaani, jambo ambalo lilikuwa likichangia kuongeza gharama na kusababisha ugumu wa maisha.

Vailethi Masunzu, mkazi wa kijiji cha Nyangwijima wilaya ya Kakonko naye anatoa malalamiko kama hayo kwamba kwa muda mrefu wameteseka na shida ya maji baada ya mradi wa maji hapo kijijini kuacha kutoa maji.

Anasema tatizo lilikuwa ni changamoto ya pampu ya kusukuma maji na hivyo kulazimika kutegemea maji ya mtoni na kwenye madimbwi wakati wa mvua, jambo ambalo lilichangia homa za matumbo za mara kwa mara kwa wananchi.

Lakini Robert na Vaileth, kwa nyakati tofauti wanasema changamoto iliyowakabili kwa muda mrefu imekwisha baada ya miradi ya maji kukamilika katika maeneo yao na shukrani wanazipeleka kwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA).

Robert anasema huduma ya maji sasa inawafikia karibu na makazi yao baada ya kukamilika kwa mradi wa maji wa Mabamba/Mkarazi.

Lakini kwa Estaher Daniel, mkazi wa kijiji cha Kibwigwa wilaya ya Buhigwe, anasema wao bado wanahangaika na shida ya maji kutokana na kijiji chao kuendelea kutopata huduma ya maji ya bomba.

“Zipo taarifa za kuanza kutekelezwa kwa mradi wa maji katika kijiji chetu mwaka huu. Tunasubiri kwa hamu ili kutuondolea hii adha ya maji,” anasema.

Kimsingi, Mkoa wa Kigoma upo kwenye mkakati mkubwa wa kukabiliana na matatizo ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji ili kuunga mkono juhudi za serikali za kumtua mama ndoo.

Ni katika muktadha huo, Meneja wa Ruwasa mkoa Kigoma, Mathias Mwenda, anaeleza kuwa kwa sasa hali ya upatikanaji wa maji mkoa humo imedikia asilimia 67.

Anasema hadi kufikia mwisho wa Februari, 2021, Ruwasa Mkoani Kigoma ilikuwa imekamilisha ujenzi wa miradi 31 yenye thamani ya shilingi bilioni 11.4 inayokadiriwa kuhudumia Watanzania wapatao 233,067.

Sambamba na ukamilishaji wa miradi hiyo, Ruwasa Kigoma inaendelea na utekelezaji wa jumla ya miradi 28 ya ujenzi ambayo iko katika hatua mbalimbali inayotegemewa kukamilika kabla ya mwezi Juni mwaka huu.

Mwenda anasema katika mahojiano na gazeti hili kwamba katika kipindi cha miaka mitatu tangu wakala huo kuundwa wamejiwekea malengo ya kuondoa tatizo la maji na kuhakikisha huduma hiyo inafika karibu na makazi ya watu.

“Wakala wetu kwenye ngazi za mikoa na wilaya tunafanya tafiti ya vyanzo vya maji na kuibua miradi kwa ajili ya maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji,” anasema Mwenda.

Mkoa wa Kigoma una jumla ya vijiji na mitaa 414 inayosimamiwa na Ruwasa na kati ya hivyo, vijiji 118 havina huduma ya maji hivyo kupitia Programu Endelevu ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini, Ruwasa Mkoa wa Kigoma inategemea kutekeleza jumla ya miradi 18 katika mwaka huu wa fedha.

Miradi hiyo kwa sasa ipo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji ambapo kati yake ipo miradi ya zamani ambayo imefufuliwa, iliyoboreshwa na miradi mipya.

Mwenda anasema katika mwaka huu wa fedha 2021/22, wakala unategemea kutekeleza miradi 26 itajayohudumia vijiji 60.

Anasema kutekelezwa kwa miradi hiyo kutaufanya mkoa kufikia asilimia 85 ya upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Miradi kichefuchefu

Kwa mujibu wa meneja huyo, Ruwasa Kigoma ilirithi miradi minane kutoka halmashauri za wilaya ambayo ilikua na changamoto za kutokutoa huduma licha ya miradi hiyo kukamilika. Miradi hiyo ni Kidududye, Katanga/Ilabiro, Nyagwijima, Muhange, Kiga, Kalinzi, Nyarubanda, Nkungwe na Kandaga.

“Mpaka sasa changamoto za miradi mitano ya Kiduduye, Katanga/Ilabiro, Nyagwijima, Muhange na Nkungwe zimetatuliwa na kwa sasa inafanya kazi vizuri baada ya kuifanyia maboresho na kubadilisha aina ya nishati iliyokuwa ikitumika kusukuma maji kutoka matumizi ya jenereta zinazotumia mafuta ya dizeli na kwa sasa kumefungwa umeme jua,” anasema.

Aidha anasema mradi mmoja wa Kalinzi bado una changamoto ya uendeshaji kutokana na tatizo la umeme kukatika mara kwa mara kwenye eneo hilo huku miradi miwili ya Nyarubanda, wilaya ya Kigoma na Kiga wilaya ya Kakonko juhudi Shirika la ugavi wa umeme (Tanesco) zinaendelea kuunganisha umeme kwenye miradi hiyo.

“Pamoja na miradi mingi ambayo Ruwasa tunaibua, kubuni, kutafiti na kutekeleza ipo miradi ya muda mrefu maarufu kama miradi kichefuchefu ambayo tumeamua kwa nguvu moja kuhakikisha inamalizika na kuanza kutoa huduma,” anasema na kwamba wanatarajia kutekeleza miradi 18 katika mwaka wa fedha 2020/2021.

Miradi hiyo inatekelezwa katika vijiji vya Titye, Kitema, Kigembe, Mkigo, Kiziba, Kazuramimba, Sigunga, Mlela, Mpeta, Kashagulu, Buyezi, Migongo, Kilelema, Mwayaya, Nkuba, Mugunzu, Kinonko, Njomlole na Kanyonza.

Anasema kutekelezwa kwa miradi hii inayotegemea kuhudumia jumla ya wakazi wapato 140,726 sawa na ongezeko la asilimia 6.7 kutasababisha ongezeko la wanaopata maji kufikia asilimia 73.3.

Mradi wa Ziwa Tanganyika.

Mwenda anasema wanatarajia kuanza kutekeleza mradi mkubwa wa kutoa maji ziwa Tanganyika na kuyapeleka kwenye wilaya zote za mkoa Kigoma.

Kwa sasa anasema utafiti unafanyika wa kutoa maji hayo kutoka Kigoma Mjini kupeleka kijiji cha Munanila wilaya ya Buhigwe ambalo ndiyo eneo lenye mwinuko mkubwa kuliko yote mkoani Kigoma.

Kutoka Munanila anasema kuwa maji hayo yanaweza kufika katika vijiji vyote vya Wilaya ya Buhigwe na Kasulu kwa mserereko na baadhi ya vijiji vya Kigoma na Uvinza. Lakini anasema kwa wilaya za Kibondo na Kakonko hali inaonesha kunahitajika mashine za kuyasukuma ili yaweze kufika katika wilaya

hizo.

“Utafiti wa awali unaonesha umbali kutoka Kigoma mpaka kijiji cha Munanila ambapo kunategemewa kujengwa tangi kubwa la kuhifadhia maji ni kilometa 59 na kutoka Munanila mpaka Wilaya ya Kakonko kuna umbali wa kilometa 238. Tathmini ya mradi huu bado inaendelea na utekelezaji wake utakua ni wa awamu,” anasema mhandisi huyo.

Mhandisi wa Ruwasa wilaya ya Kigoma, Leon Mombeki anasema kuwa kutekelezwa kwa mradi huo maji ya ziwa Tanganyika, kutamaliza tatizo la maji katika halmashauri hiyo hasa kutokana na matatizo yanayovikumba vyanzo vya maji na uharibifu wa vyanzo hivyo.

Mhandisi wa maji wa wilaya Buhigwe, Festo Mpogole nasema kwa sasa vijiji 15 havina huduma ya maji ya bomba na kwamba kutekelezwa kwa mradi wa kutoa maji ziwa Tanganyika kutaondoa changamoto hiyo.

Meneja wa Ruwasa wilaya ya Kakonko, Benjamen Bryton anasema kuwa wilaya hiyo imefanikiwa kuongeza upatikanaji wa maji kutoka asilimia 48 hadi 73 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Bryton anasema katika kipindi hicho miradi 12 ilitekelezwa ambapo kati yake miradi mipya ilikuwa mitatu, umaliziaji mradi ulikuwa mmoja na miradi minane ilikuwa ya ukarabati ambapo

vituo vya maji 564 vinatoa huduma na watu 130,000 wanapata maji.

Anasema bado changamoto ya upatikanaji wa maji ipo kwa vijiji 14 kati ya vijiji 44 vya wilaya ya Kakonko.

Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma ni moja ya maeneo yaliyokuwa na malalamiko makubwa ya shida ya maji ambapo ni vijiji 25 ndiyo vinapata huduma hiyo kati ya vijiji 50.

Hata hivyo, wilaya imefanikiwa kukabiliana na hali hiyo kwa kupeleka huduma ya maji kwa wanachi kwa asilimia 83 kwa kutumia vyanzo mbalimbali ikiwemo visima virefu, vifupi na mabomba

Mhandisi wa maji wilaya Kibondo, Mohamed Almasi anasema kuwa wilaya imejikita kumaliza miradi iliyokwama na kwa sasa tayari mradi wa kijiji cha Minyinya umekamilika na kuanza kufanya kazi baada ya kukaa miaka mitano bila kutoa huduma.

Akielezea utekelezaji wa mradi mkubwa wa kutoa maji ziwa Tanganyika Almasi anasema kuwa mradi huo utakuwa na manufaa kwao lakini pia kwa mji wa Kibondo.

Pamoja na kazi kubwa ya utekelezaji wa miradi, Meneja Mwenda anasema kuwa usimamizi wa utoaji wa huduma za maji mkoani humo unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uharibifu wa vyanzo vya maji hasa kutokana na shughuli za kibinadamu na uchache wa watalaamu.

“Katika kukabiliana na tatizo la uchafuzi wa vyanzo vya maji, Ruwasa Mkoa wa Kigoma imekua ikishirikiana na Bodi ya Bonde la Ziwa Tanganyika kutoa elimu na kuchukua hatua stahiki pale inapohitajika kulingana na Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji Namba 11 ya Mwaka 2009,” anasema.

Pamoja na hilo anasema kuwa kuna mwitikio mdogo wa jamii kuchangia gharama za huduma ya maji.

Anasema katika kupunguza changamoto ya gharama na kuboresha huduma baadhi ya miradi inayotumia majenereta yanayoendeshwa kwa nishati ya mafuta ya dizeli wameibadilisha kwa kufunga umeme wa Tanesco au umeme-jua.

Chanzo: www.habarileo.co.tz