Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ruvuma yapangia shule watoto wote waliofaulu la 7

E587c47014dacffa57b8a5008060eeac Ruvuma yapangia shule watoto wote waliofaulu la 7

Mon, 21 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

Mkoa wa Ruvuma umefanikiwa kuwapangia shule za sekondari watoto wote 27,136 waliofaulu mtihani wa kuhitimu darasa la saba mwaka 2020.

Akizungumza kwenye kikao cha kutangaza wanafunzi waliochaguliwa kuanza kidato cha kwanza mwaka 2021, kilichofanyika ukumbi wa Manispaa ya Songea, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme alisema mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa tisa nchini iliyofanikiwa kuwapangia shule watoto wote waliofaulu.

Mndeme alisema kati ya wanafunzi waliofaulu wavulana ni 12,799 na wasichana ni 14,336 na kwamba ufaulu huo ni sawa na asilimia 78.50 ya wanafunzi waliohitimu mwaka 2020.

Hata hivyo alisema mwaka 2019 ufaulu wa darasa la saba ulikuwa ni asilimia 83.70 hivyo mwaka huu ufaulu umeshuka kwa asilimia 5.2 wakati mwaka jana wanafunzi waliofaulu walikuwa 32,298 kati yao wavulana 15,236 na wasichana 17,062.

“Tuhakikishe kuwa watoto wote waliofaulu wanaripoti shule mara baada ya shule kufunguliwa Januari 2021 na wazazi watakaokiuka maelekezo haya wachukuliwe hatua,Isiwepo sababu yoyote itakayomzuia mwanafunzi aliyefaulu kuanza shule,”alisisitiza.

Mndeme pia alipiga marufuku michango ya shule inayokwenda kinyume na maelekezo yaliyotolewa na serikali kupitia waraka wa elimu bila ada.

Mkuu huyo wa mkoa aliwapongeza viongozi na watendaji wote wa serikali kwa kufanya elimu kuwa kipaumbele cha kwanza kwa kuhakikisha kuwa miundombinu ya shule inajengwa.

“Ninaagiza mwakani kusiwepo na upungufu hata wa chumba kimoja cha darasa na samani zake, pia nazipongeza Halmashauri za Madaba na Manispaa ya Songea kuwa na ziada ya jumla ya madarasa 21,” alisema Mndeme.

Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Stephen Ndaki aliwaagiza maofisa elimu na wadau wote wa elimu kusimamia taaluma ili ufaulu uweze kuongezeka na kuufanya mkoa wa Ruvuma kuwa na ufaulu wa juu.

Alizipongeza kamati za mitihani katika shule kwa kufanya kazi kubwa mwaka huu, hata hivyo ameshangazwa katika kipindi cha mitihani baadhi ya walimu na wanafunzi wao kushindwa kujiamini.

Ndaki alisema katika utafiti mdogo uliofanyika umebaini sehemu kubwa ya wasimamizi wa taaluma shuleni hawafanyakazi yao kikamilifu ya kusimamia walimu ili waweze kutoka na matokeo mazuri.

“Ukiangalia matokeo ya mwaka 2020 utabaini kuwa ni wanafunzi wachache waliofikia ufaulu wa daraja A, wengi wanapata C na B alama ambazo haziwezi kuwafanya watoto wetu waweze kushindana kwenda kwenye shule za bweni nje ya Mkoa wa Ruvuma,” alisema Ndaki.

Chanzo: habarileo.co.tz