Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ruvuma yakamilisha vyumba 500 vya madarasa

Fde452a1ba029789ea5be41a6f91e1a9.jpeg Ruvuma yakamilisha vyumba 500 vya madarasa

Sat, 1 Jan 2022 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mkoa wa Ruvuma kupitia halmashauri zake nane, umekamilisha ujenzi wa vyumba 500 vya madarasa vilivyojengwa kwa fedha ya mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Covid-19.

Hayo yalisemwa jana na Mkuu wa mkoa huo, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa madarasa katika kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa wa Ruvuma (RCC), kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano ya Manispaa ya Songea.

Alisema kukamilika kwa vyumba hivyo kunatoa fursa kwa wanafunzi waliochaguliwa kuanza kidato cha kwanza mwaka huu, kuwa na mahali safi na salama kwa ajili ya safari yao ya masomo.

Alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuupatia mkoa huo zaidi ya Sh bilioni 10 kwa ajili ya kujenga vyumba vya madarasa 500 na mabweni matatu ya shule zenye wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

Aidha, amelipongeza wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri kwa kazi nzuri ya kusimamia ujenzi wa madarasa hayo na kuwataka kuendelea kusimamia vyema miradi mingine ya maendeleo inayotekelezwa katika wilaya zao.

Jenerali Ibuge, alitoa wito kwa wadau wenye dhamana ya kuwekeza katika elimu ya watoto kuweka mikakati mizuri ya ufundishaji, kupambana na utoro na mimba za utotoni na miundombinu bora ya shule ili watoto kuanzia madarasa ya awali, shule za msingi na sekondari waendelee kufanya vizuri.

Katika hatua nyingine, Wabunge wa Mkoa wa Ruvuma walimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kumteua Ibuge kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.

Akizungumza kwa niaba ya wabunge hao, Mbunge wa Nyasa, Stella Manyanya alisema tangu Rais Samia alipomteua Jenerali Ibuge kuwa mkuu wa mkoa wa Ruvuma ameleta mabadiliko makubwa na uwajibikaji kwa watumishi wa umma.

Chanzo: www.habarileo.co.tz