Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rungu la DC Hai latua kwa Halmashauri, DED aomba radhi

77320 Dc+pi

Thu, 26 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Hai. Halmashauri ya wilaya ya Hai  mkoani Kilimanjaro nchini Tanzania jana Jumatano Septemba 25, 2019 ilionja machungu ya kukatiwa umeme, baada ya mkuu wa wilaya hiyo, Lengai Ole Sabaya kuagiza ikatiwe umeme ili waone uchungu wa kukosa nishati hiyo.

Amri hii ya Sabaya aliitoa kutokana na kuchukizwa na kitendo cha Halmashauri kutolipa bili ya umeme ya Sh262,000 na kusababisha soko kuu la Bomang’ombe kukatiwa huduma ya umeme.

Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), wilaya ya Hai, Theodory Hillal alisema soko hilo lilikuwa linadaiwa malimbikizo ya umeme ya Sh262,000 hivyo wakalazimika kukata umeme.

Sabaya aliyefanya ziara ya ghafla katika soko hilo baada ya kupokea malalamiko ya wafanyabiashara, alisema ni aibu kwa Halmashauri kukusanya ushuru halafu isilipie umeme.

"DED (mkurugenzi) wewe watu wako kwa mfululizo mnakuja kukusanya pesa kwa miezi mitatu, mnasahauje kulipa bili kupitia pesa hizo zao? Hili nalo Rais (John Magufuli) asimamishwe aambiwe?” alihoji Sabaya.

Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Yohana Sintoo alipopewa nafasi alimuomba radhi mkuu huyo wa wilaya na wafanyabiashara waliokuwepo hapo, lakini Sabaya akaagiza umeme ukatwe.

Pia Soma

Advertisement
“Mheshimiwa mkuu wa wilaya naomba niwaombe radhi hawa wananchi. Haukupaswa kurudi mara ya pili hapa. Umeme utawaka leo hapa sokoni,” alisema Mkurugenzi huyo mbele ya wananchi.

“Mimi na wewe tuwaombe hawa wananchi radhi ila wakati huo huo nakuagiza Meneja wa Tanesco kakate umeme ofisi ya mkurugenzi na uwashe hapa sokoni na alipe deni hilo,” alisema Sabaya.

“Na alipe bili za miezi sita ijayo umeme hapa uwake leo na Go ahead (kibali) ya kurudisha umeme kwa DED nitakupa baada ya kuona risiti kuwa ameshalipa huo umeme,” alisisitiza

“Na kwa kuwa ofisi yangu iko kwenye jengo hilo tukapambane wote na hilo joto la kuwapuuza hawa wananchi tunaoambiwa kila siku kuwasikiliza na kuwahudumia,”

Mkuu wa wilaya alisema kuanzia hiyo jana, endapo kutatokea Halmashauri imeshindwa kulipa umeme katika masoko inayokusanya ushuru, masoko hayatakatiwa umeme bali ofisi za Halmashauri.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz