Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rukwa yapata mafanikio chanya utoaji haki

267f4c55695ca3a9701432bf1123fc5f.jpeg Rukwa yapata mafanikio chanya utoaji haki

Sat, 29 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKOA wa Rukwa umeeleza mafanikio chanya katika utoaji haki, mafanikio ambayo yamewafanya wananchi wa mkoa huo kuishi kwa amani na usalama na hivyo kuweka mazingira rafiki kwa maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla.

Hayo yamo katika taarifa ya mkoa huo kuhusu hali ya utekelezaji wa hakijinai iliyoainisha mafanikio na changamoto.

Taarifa hiyo ilisomwa na Wakili Frida Hava wakati wa kikao kati ya Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Profesa Sifuni Mchome, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Laurean Ndumbaro na Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk John Jingu, na wadau wa hakijinai mkoani Rukwa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mafanikio hayo yamechangiwa pamoja na mambo mengine na uwepo wa ushirikiano wa idara, ofisi na taasisi mbalimbali zinazoisaidia mahakama katika kutenda haki.

Baadhi ya ofisi hizo ni kuanzishwa kwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na Huduma kwa Jamii na Sheria ya Majaribio na Ujenzi wa Tabia.

Iliongeza kuwa malalamiko mengi ya wananchi yamekuwa yakishughulikiwa na vyombo hivyo vya utoaji haki kwa weledi na ufanisi mkubwa na hivyo kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi ambayo yangefikishwa katika ofisi za serikali na kushughulikiwa pasipo kufuata misingi ya utoaji wa haki.

Aidha, mkoa huo unajivunia kuendelea kupungua kwa msongamano wa wafungwa gerezani hasa baada ya kuanzishwaji wa Huduma kwa Jamii na Sheria ya Majaribio ya Ujenzi wa Tabia mwaka 2018, kwani hadi sasa mkoa una wataalamu wawili wanaoshughulika na utoaji wa huduma hiyo.

“Kwa rejea, tangu mwezi Agosti, 2018 hadi Mei, 2021 Idara ya Huduma za Uangalizi imefanikiwa kutoa jumla ya wafungwa wa kifungo cha nje 136. Kwa kuwa idara hii inahamasisha utoaji wa adhabu mbadala imesaidia kupunguza gharama kwa serikali katika kuwahudumia wafungwa na kuwasaidia wahalifu wadogo wasiende kujifunza mbinu mpya za uhalifu pindi wanapokuwa gerezani,” ilibainisha taarifa hiyo.

Pamoja na mafanikio hayo, taarifa ilieleza mkoa unakabiliwa na changamoto kadhaa katika utekelezaji wa hakijinai.

Ilizitaja baadhi ya changamoto hizo ni baadhi ya vyombo vinavyohusika kutoa haki kulalamikiwa kujihusisha na rushwa na kusababisha haki ya wananchi kupotea kabisa au kuchelewa kabisa.

Pia baadhi ya vyombo vya utoaji haki kuingiliwa na vyombo vingine visivyo na mamlaka ya kutoa haki mfano Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) huingiliwa utendaji wake na watendaji wa serikali.

Akijibu baadhi ya changamoto hizo ikiwamo ya baadhi vyombo vya utoaji haki kuingiliwa na vyombo visivyo na mamlaka ya utoaji haki, Profesa Mchome ametaka jambo hili liachwe mara moja na kila chombo kitekeleze majukumu yake bila kuingilia chombo kingine. Amesisitiza weledi, maadili na miongozo ya utumishi wa umma kutumika.

Chanzo: www.habarileo.co.tz