Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rukwa kuunda kikosi kubaini kuporomoka kwa ufaulu

C88cca49dc5096023d26d75796e7f826 Rukwa kuunda kikosi kubaini kuporomoka kwa ufaulu

Sat, 9 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa, Benard Makali kuunda kikosi kazi cha wataalamu ili kubaini sababu za kuporomoka kwa ufaulu wa Mtihani wa Taifa wa Kuhitimu Elimu ya Msingi 2020.

Alisema kikosi kazi hicho kifuatilia shule kwa shule, kubaini changamoto walimu wanazokabiliana nazo, miundombinu ya shule na mazingira.

Wangabo alitoa maagizo hayo alipokuwa akizungumza na wadau wa elimu, wakiwemo wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, walimu wakuu, wakuu wa shule na maofisa elimu.

Akifafanua, alisema kuwa ametoa maagizo hayo kufuatia mfululizo wa matokeo ya mtihani wa kuhitimu darasa la saba kwa miaka sita kuonesha ufaulu wa mkoa umekuwa ukipanda tangu 2015 hadi 2019, lakini tangu 2020 ufaulu umeshuka kwa asilimia 0.03 ukilinganishwa na 2019 ambapo ufaulu ulikuwa asilimia 81.01. Alisema mwaka 2020 ufaulu umekuwa asilimia 80.03.

“Hii si dalili nzuri kabisa sijafurahishwa nayo inaashiria kuporomoka kwa ufaulu huenda kunasababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo usimamizi hafifu katika ngazi mbalimbali kuanzia nyumbani mpaka shuleni na kusababisha kushuka kwa ufaulu,” alieleza.

Aliwaagiza maofisa elimu wa ngazi zote, kuongeza usimamizi thabiti wa elimu kwa kufuatilia shughuli za ufundishaji shuleni.

“Katika hili nisisitize walimu wakuu, wakuu wa shule na maofisa elimu kata kusimamia kikamilifu ufundishaji madarasani,” alisema. Aliwataka pia maofisa elimu waongeze ufuatiliaji wa taaluma shuleni ili kuhakikisha walimu wanafundisha kwa kufuata mitaala na kukamilisha ufundishaji wa mada zote kwa wakati na kutoa mazoezi ya kutosha ili kuwaandaa wanafunzi vyema.

Kwa upande wa wazazi na walezi, aliwataka kushirikiana na walimu katika shughuli za kitaaluma kwa kuwasimamia wanafunzi kikamilifu wawapo nyumbani na kuhudhuria shuleni kwa mujibu wa ratiba na mihula ya shule.

“Nafahamu kuwa pamoja na wanafunzi 16,540 kuchaguliwa kujiunga kidato cha kwanza 2021 kwa awamu ya kwanza wapo wanafunzi 564... wanafunzi 310 katika Manispaa ya Sumbawanga na 254 wilaya ya Kalambo ambao hawakuchaguliwa katika awamu hii kutokana na kukosekana kwa vyumba vya madarasa, naagiza wakuu wa wilaya za Kalambo na Sumbawanga kusimamia kikamilifu upatikanaji wa vyumba vya madarasa vinavyohitajika na wanafunzi waliokosa nafasi ili kabla ya Februari 28,mwaka huu wajiunge na kidato cha kwanza,” aliagiza.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga, Jacob Mtalitinya alisema halmashauri hiyo inakabiliwa na upungufu wa madawati 980. Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Calorious Msungwi alisema wilaya hiyo ina upungufu wa vyumba vya madarasa 18.

Chanzo: habarileo.co.tz