Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rufaa ya Wakili Mwale na wenzake yagonga ukuta

9927 Pic+mwale

Mon, 25 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakili maarufu jijini Arusha, Median Mwale anayekabiliwa na kesi ya jinai na wenzake watatu, wamegonga mwamba katika Mahakama ya Rufani baada ya rufaa yao kutupiliwa mbali kutokana na kasoro za kisheria.

Rufaa hiyo imetupwa kutokana na kasoro hizo katika taarifa yao ya kusudio la kukata rufaa.

Katika uamuzi wake uliotolewa na jopo la majaji watatu; Mbarouk Mbarouk (aliyeongoza jopo), Stella Mugasha na Jacobs Mwambegele, mahakama ilitupa rufaa hiyo baada ya kukubaliana na hoja za pingamizi la awali la Serikali.

“Mahakama hii katika uamuzi wa kesi mbalimbali imetamka kuwa kushindwa kuelezea kiini cha uamuzi/amri ya Mahakama Kuu ambayo inakusudiwa kukatiwa rufaa katika taarifa ya kusudio la kukata rufaa kunaifanya rufaa inayokusudiwa kutokuwa na maana.

“Rufaa inatupiliwa mbali kwa kutokuwa na maana.” imesisitiza Mahakama ya Rufani katika uamuzi huo ambao Mwananchi imeiona nakala yake.

Mwale na wenzake Don Bosco Gichana, Boniface Mwimbwa na Elias Ndejembi wanaokabiliwa na kesi Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, walikata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu kuuruhusu upande wa mashtaka kuwafutia mashtaka kabla ya kuwakamata tena.

Katika kesi ya awali namba 61 ya mwaka 2015, Wakili Mwale na wenzake walikuwa wanakabiliwa na jumla ya mashtaka 44 yakiwemo ya kula njama, kutenda kosa, utakatishaji fedha, kughushi, kuwasilisha hati za uongo na kumiliki mali zinazodaiwa kupatikana isivyo halali.

Wakati kesi hiyo ikiwa imeshaanza kusikilizwa hadi shahidi wa pili wa upande wa mashtaka, upande wa mashtaka uliomba kuwafutia mashtaka chini ya kifungu cha 91 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Upande wa utetezi kupitia kwa Wakili Albert Msando ulipinga maombi hayo ya upande wa mashtaka pamoja na mambo mengine ukidai kuwa uamuzi huo si wa nia njema, bali uligubikwa na nia mbaya kwa lengo la kuendelea kuwaweka mahabusu washtakiwa.

Mahakama katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji David Mrango Oktoba 31, 2017, ilitupilia mbali pingamizi hilo la upande wa utetezi na badala yake ikakubaliana na maombi ya upande wa mashtaka.

Kutokana na uamuzi huo, upande wa mashtaka uliwafutia mashtaka washtakiwa hao, lakini ukawakamata na kuwafungulia upya mashtaka hayo.

Wakili Msando alilieleza Mwananchi jana kuwa upande wa mashtaka uliamua kutumia utaratibu huo kuwafutia mashtaka baada ya kushindwa kuingiza mahakamani nyaraka muhimu za ushahidi kupitia kwa mashahidi wake wawili waliokuwa wameshatoa ushahidi.

Hivyo walikata rufaa Mahakama ya Rufani, lakini mjibu rufani (mkurugenzi wa mashtaka - DPP), aliwasilisha pingamizi la awali akibainisha kasoro za taarifa hiyo ya kusudio la kukata rufaa.

Wakati wa usikilizwaji wa pingamizi hilo, mjibu rufaa (DPP) aliwakilishwa na wakili wa Serikali mkuu, Oswald Tibabyekomya akisaidiana na mawakili wa Serikali waandamizi; Hashimu Ngole na Awamu Mbagwa.

Warufani waliwakilishwa na mawakili Alex Mgongolwa, Godwin Simbangwilimi, Omari Idd Innocent Mwanga na Jeremiah Mtobesya.

Katika pingamizi hilo, Wakili Mbagwa alidai kuwa taarifa ya kusudio la kukata rufaa ina upungufu wa kisheria kwa kuwa haielezi kiini cha uamuzi wa mahakama unaokusudiwa kukatiwa rufaa.

Alidai kuwa badala yake katika muktadha wa taarifa hiyo, warufani wanakata rufaa dhidi ya kitendo cha kuondolewa mashtaka dhidi yao (nolle prosqui), kulikofanywa na DPP ambacho si kiini sahihi cha uamuzi unaokusudiwa kukatiwa rufaa.

Wakili Mbagwa alidai kuwa kutoeleza kiini cha uamuzi unaokatiwa rufaa kinakinzana na matakwa ya lazima ya kanuni ya 68(2) ya Kanuni za Mahakama ya Rufani za mwaka 2009.

Akijibu hoja hizo, Wakili Mgongolwa aliiiomba mahakama itupilie mbali pingamizi hilo akidai kuwa halina msingi wa kisheria, huku akisisitiza kuwa hoja za kukatiwa rufaa kwenye uamuzi wa Jaji Mrango zimeelezwa wazi kwenye taarifa ya kusudio la kukata rufaa.

Wakili Mgongolwa alisisitiza kuwa taarifa ya kusudio la kukata rufaa sharti isomwe katika muktadha wake na kwamba, si kila kasoro au kutotimiza matakwa ya kanuni kunaweza kusababisha rufaa yote kuwa na maana.

Chanzo: mwananchi.co.tz