Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ruangwa walivyofunzwa namna ya kunufaika na uziduaji madini

Cf5dd997a5ef0648157a9bd485f749f5 Ruangwa walivyofunzwa namna ya kunufaika na uziduaji madini

Tue, 18 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

HALMASHAURI ya wilaya ya Ruangwa ni miongoni mwa Halmashauri sita ambazo zinaunda Mkoa wa Lindi, zingine ni Kilwa, Lindi mjini, Lindi Vijijini, Liwale na Nachingwea. Wilaya hii iliyopo kusini magharibi mwa Mkoa wa Lindi sasa inajulikana zaidi kutokana na kuwa na madini ya aina mbalimbali.

Aina ya madini ya vito vya thamani yaliyopo ni pamoja na graphite, green tomalin/garnet, red garnet, blue sapphire, rhodolites, emeralds, pigment materials (Rangi ya puti), aquamarine na alexandrite.

Kutokana na wingi wa madini yaliyobainika kuwapo na mbio zinazofanywa za kuwekeza na kwa kujua kwamba madini yanaweza kuleta migogoro katika familia na jamii, Mtandao wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Lindi (LANGO) kwa ufadhili wa shirika la Open Society Initiative for Eastern Africa (OSIEA) Tanzania, limeendesha elimu ya kuonesha wajibu wa wanajamii na watoa uamuzi kuhusu mustakabali wa jamii na miradi hiyo.

Akizungumza kuhusiana na mradi huo, Mkurugenzi wa Lango, Michael Mwanga anasema lengo la mradi ni kuimarisha ushiriki wa wananchi, uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa mapato ya tozo ya huduma katika sekta ya uziduaji, hasa katika kipidni hiki ambacho serikali inawahimiza waliochukua leseni mkoani Lindi na hasa Ruangwa kuacha kuzificha na badala yake kuendelea kuzifanyia kazi ili kulipa tozo zinaozohusika na kuendeleza jamii .

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula mwaka jana akiwa katika ziara ya kutembelea eneo linalotarajiwa kuanzishwa miradi wa uchimbaji na uchenjuaji madini ya kinywe (graphite) wa Kampuni ya Lindi Jumbo uliopo Kijiji cha Matambarare, Wilayani Ruangwa, Mkoani Lindi, alisisitiza haja ya kila mwenye leseni kuratibu vyema eneo lake na kulifanyia kazi.

Katika ziara hiyo ambayo Profesa Kikula aliambatana na Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Lindi, Jeremiah Hango pamoja na Maafisa wengine kutoka Tume ya Madini; Iddi Msakuzi, Daudi Ntalima, Dickson Joram na Fadhili Kitivai alisema kupitia ziara hiyo amebaini ukiukwaji wa Sheria ya Madini ambapo wawekezaji wamekuwa wakishikilia leseni za utafutaji wa madini bila kuziendeleza kwa kipindi kirefu.

“Kitendo cha kushikilia leseni za utafutaji madini bila kuziendeleza ni makosa kisheria na ni dhahiri kuwa Serikali inakosa mapato yake stahiki,” alisisitiza Profesa Kikula. Kwa sasa wenye leseni wamekuwa wakizinafanyia kazi hoja hizo kwa kasi kubwa na wengi wapo katika maeneo yao baada ya kukamilisha taratibu za tathmini kwa ajili ya ulipaji wa fidia.

Mwenyekiti huyo pia alibaini kuwapo kwa migogoro baina ya kampuni kadhaa na wazawa na kuagiza kuacha mwenendo huo usiokuwa na afya katika maizngira ya kazi, ustawi wa jamii na mapato kwa taifa.

Kutokana na mahitaji makubwa ya kuleta maelewano ili kuepusha shari na kupunguza migogoro kati ya wadau wote wa madini wakiwemo wananchi, watendaji na wawekezaji, Mkurugenzi wa Lango, Mwanga anasema mafunzo waliyoyapeleka Ruangwa yamelenga kuweka mazingira ya uwekezaji salama kwa kuwawezesha wadau wote waliopo Ruangwa kufahamu kwa kina sera na sheria zinazohusu sekta ya madini na uziduaji ili kuwezesha maendeleo yao na ya taifa kwa ujumla.

Ofisa mradi wa kuimarisha ushiriki wa wananchi, uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa mapato ya tozo ya huduma katika sekta ya uziduaji madini na gesi asilia wa Lango, Aina Pero anasema mafunzo hayo yaliyoshirikisha watendaji kata, wenyeviti wa vijiji na waraghbishi yalilenga kuwapa uelewa shirikishi ambao utawezesha wananchi kunufaika na uwekezaji katika madini hayo na pia kuwawezesha wawekezaji kupata faida waliyokusudia.

"Tunawaelimisha wadau hawa ili waende nao kuelimisha wenzao wanaowazunguka kwenye maeneo walikotoka yenye madini ili kuondoa dhana dhaifu inayohusu madini katika mapato na faida ya wananchi," anasema Pero.

Pero anasema mafunzo hayo yaliyoshirikisha watendaji kata, wenyeviti wa vijiji na waraghbishi kutoka Halmashauri ya Ruangwa na Kata za Mbekenyera, Matambalale na Chunyu yamelenga kuwaandaa wananchi kuwa tayari na kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wa madini huku wakitambua haki zao.

Katika mafunzo hayo ya siku mbili wadau hao walipata fursa ya kufahamu sera na sheria mbalimbali zinazosimamia sekta ya uziduaji nchini. Wadau walifundishwa Sera ya Ushiriki wa Wananchi (Local Content Policy 2014), Sheria ya Madini ya mwaka 2017, Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika sekta ya uziduaji ya mwaka 2015, sheria ya Usimamizi wa Mapato sekta ya uziduaji ya mwaka 2015, na sheria ya ulipaji fidia ya ardhi kupisha shughuli za uwekezaji katika sekta ya uziduaji.

"Kama tunavyofahamu sote kwamba raslimali madini ni miongoni mwa zile ambazo hazijirudii kadri shughuli za uziduaji wake zinavyofanyika na kuvunwa. Kwa mantiki hiyo ni jambo jema kuhakikisha kwamba wadau mbalimbali wanakua na uwelewa wa pamoja na wa kutosha kuhusu sera na sheria zinazosimamia sekta hii muhimu ili kuleta tija kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla," anasema Mkurugenzi wa Lango, Mwanga.

Anasema nia ya asasi yake ni kuhakikisha kwamba kupitia mafunzo hayo wadau wanapata fursa ya kufahamu kuhusu sera ya ushiriki wa wananchi kwenye sekta hiyo.

"Tumekuja Ruangwa kwa kuwa kuna uwekezaji mkubwa kwenye maliasili, vijiji vingi vina madini. Tumeanza na kata tatu ili kuwaelimisha wajue manufaa ya uwekezaji katika madini na wajibu wao. Shirika linalenga kutengeneza mazingira mazuri kwa wenyeji na namna halmashauri kujua wanavyoweza kunufaika. Kuwaandaa wadau wanaohusika katika uendeshaji kwa kuwa na elimu ya kuwezesha kutambua na kuondoa malalamiko ya wanajamii kuhusu sekta ya uziduaji," anasema Mwanga.

Anasema ni nia ya taasisi yake ni kusaidia wananchi kupambana na umaskini kwa namna bora kabisa, kwa kuwekea mazingira ya maelewano na uwajibikaji katika uziduaji madini kwa kuangalia sera na sheria na usimamizi wa vitu hivyo ili kila mmoja anufaike.

"Ni ukweli usiopingika kwamba ushiriki na ushirikishaji wa wananchi katika tasnia ya uziduaji ni jambo muhimu sana ambalo litasaidia kuimarisha umiliki na kupunguza matarajio na matumaini makubwa ya kufaidika na tasnia husika miongoni mwa wananchi kinyume na hali halisi. Hivyo basi ni muhimu kwetu wadau na jamii kwa ujumla kuweza kuelewa sera hii inazungumza nini hususani kwenye suala la ushiriki wa wananchi kwenye sekta," anasema Mwanga.

Mafunzo haya ambayo ni mapya yanaelezwa na wananchi mbalimbali kuwa yamewabadili na kuwafanya wawe na uelewa zaidi hivyo kuwa na hamu ya kwenda kutekeleza walichojifunza.

Mohamed Abdallah, Shahane Nangongo na Tatu Abdallah wanasema mafunzo hayo yamewaweka katika hali ya kutambua namna ya kushiriki katika sekta hiyo ya madini kwa manufaa yao na taifa huku wakihakikisha kwamba raslimali hizo zinazoisha zinatumika vyema kwa manufaa ya wananchi wa maeneo husika.

Rajab Rashid Mohamed, mkazi wa Mbekenyera anasema kwamba mafunzo aliyoyapata yamembadili kifikira hasa namna ya kutumia fursa zilizopo kuleta maendeleo na kujiandaa na matarajio ya umma katika kujiendeleza.

"Tumepewa nafasi ya kutambua kwamba tunahitaji kujiandaa kupata mradi kama tunataka kufaidi matunda yake kwa kujua kwamba mahitaji yapi yataweza kutolewa na wawekezaji kwetu wakianza kazi ya uziduaji. Ni jambo gani wanatakiwa kulifanya kama urejeshaji wa faida, ulipaji wa tozo na kadhalika," anasema Mohamed.

Fredrick Pasati kutoka Namungo anasema anashukuru mafunzo hayo yamewafanya kufahamu maelekezo ya kisera na kisheria kuhusu uziduaji toka utafutaji wa leseni hadi kuanza kwa kazi za kuchimba na mahusiano na wananchi wanaozunguka migodi hiyo ikiwamo fidia.

Musa Mduma anasema kwamba mafunzo yamempa ujuzi wa kudumu wa utekelezaji wa kazi zake na nini cha kufanya na anaahidi kwenda kubadili mawazo ya wananchi wenzake kuhusiana na suala la uwekezaji na faida zake kwao na kwa mwekezaji.

Tovuti ya serikali ya Mkoa wa Lindi, wilaya ya Ruangwa ina jumla ya leseni 316 za dhahabu, vito, kinywe, madini ya ujenzi, chuma, shaba, feldspar, garnet (RED & GREEN) na kadhalika.

Uchimbaji mkubwa wa madini katika Wilaya ya Ruangwa upo kwenye maeneo ya Namungo (Mbekenyera) Mandawa, Kitandi na Nambilanje. Madini ya vito vya thamani na dhahabu ndiyo madini yanayochimbwa kwa wingi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz