Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rotary Mlimani wazindua mradi wa taa za usalama UDSM

16694 Taa+pic TanzaniaWeb

Tue, 11 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Klabu ya Rotary Dar es Salaam Mlimani, imezindua mradi wa taa za barabarani za usalama kuzunguka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Mradi huo utakaogharimu zaidi ya Sh1.07 bilioni, ulizinduliwa juzi usiku katika awamu ya kwanza, huku baadhi ya wananchi na viongozi wa Serikali za mitaa inayozunguka eneo la chuo hicho wakitoa ushuhuda jinsi ambavyo taa hizo zimekuwa na manufaa kwa usalama wao.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo wa awamu ya kwanza, Rais wa Rotary Klabu ya Dar es Salaam Mlimani, Lulu Kaaya alisema kuwa chuo hicho kiko katika eneo lenye miti mingi inayosababisha giza kubwa nyakati za usiku na kwamba changamoto kubwa imekuwa ni usalama.

“Wanafunzi na wafanyakazi wanaokaa maeneo ya nje ya chuo, wanapotoka chuoni usiku wamekuwa wakiporwa baadhi ya vitendea kazi vyao kama vile kompyuta na wengine hata kujeruhiwa.” alisema Minja na kuongeza:

 “Tuliona kwamba endapo tukifanikiwa kuweka taa za barabarani itasaidia kuongeza mwanga ili kumulika maeneo yale ambayo wanafunzi na wafanyakazi wanapita wakitoka chuoni usiku watembee kwa usalama zaidi.”

Kaaya alisema ili kuhakikisha mradi huo unakuwa endelevu wameamua kutumia taa zinazotumia nguvu ya mwanga wa jua kwani hazina gharama ya kuziendesha baada ya kuzisimika.

Alisema mradi huo wameugawa katika mitaa 17 na ili kuangaza chuo chote na maeneo yanayokizunguka zinahitajika jumla ya taa 439, ambazo zitagharimu zaidi ya Sh1.078 Bilioni na taa moja mpaka kukamilika inagharimu kiasi cha Sh2,353,725.

Kaaya alisema katika awamu ya kwanza wameanza na mtaa wa Changanyikeni ambao umepewa kipaumbele kwani kuna watu wengi zaidi wanafunzi na wafanyakazi wengi zaidi na wananchi wanaotumia barabara hiyo, kwa ufadhili wa UDSM, PSPF na GEPF.

“Katika mtaa huu tumeweka taa 27 kuanzia pale barabara hii inapoanzia kwenye tawi la NBC mpaka eneo la Chuo cha Statistics (Takwimu), ambazo zimegharimu jumla ya Sh65 milioni.”, alisema Kaaya.

 

Alisema tangu waweke taa hizo takribani majuma matatu tu lakini wameshapokea shuhuda kutoka kwa wakazi wa maeneo hayo wakishuhudia kwamba taa hizo zimesaidia kuongeza usalama na akatoa wito kila anayeguswa kusaidia kukamilisha mitaa 16 iliyobaki.

Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Chuo Kikuu, Leonard Mwaikambo, alisema alikwishazungumza mara nyingi na uongozi wa UDSM kuhusu matatizo wanayoyapata wanafunzi na wakazi wa eneo hilo, kuporwa na kujeruhiwa.

“Lakini sasa tunaona mwanga na hivyo tunawashukru sana Rotary Mlimani kwa kufanikisha hili.”alisema Mwaikambo.

Mkazi wa Mbuyuni Changanyikeni, Prosper Minja alisema taa hizo walizihitaji kwa muda mrefu kwani watu wabaya wamekuwa wakitumia giza hilo kuhatarisha usalama kwa kuwakaba na hata kuwadhuru wanafunzi na wananchi, lakini kwa sasa matukio hayo hayasikiki.

Chanzo: mwananchi.co.tz