Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Robo tatu ya watoto wanaopotea ni wa kiume

39831 Pic+watoto Robo tatu ya watoto wanaopotea ni wa kiume

Mon, 4 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Septemba 26 mwaka jana Idrissa Ally alichukuliwa na watu waliokuwa ndani ya gari dogo aina ya IST, tangu wakati huo familia imebaki na majonzi na vyombo vya ulinzi vimeendelea kumtafuta bila mafanikio.

“Mtoto wetu hajapatikana kwa miezi minne sasa, tunaendelea kumtafuta tukishirikiana na Jeshi la Polisi, nawaomba Watanzania popote walipo wakimuona kijana wetu watoe taarifa.”

Kauli hiyo imetolewa na Ally Idd, baba mzazi wa kijana Idrissa Ally (13) mwanafunzi wa darasa la tano katika shule Princess Gate aliyetekwa saa 11.30 jioni wakati akicheza na wenzake eneo la Tegeta Masaiti wilayani Kinondoni.

Mtoto huyo alichukuliwa na dereva wa kiume aliyekuwa na gari aina ya Toyota IST ambaye baada ya kuwafukuza marafiki wa Idrissa, alitoa kichupa kidogo kinachodhaniwa kuwa ni dawa ya usingizi na kumpulizia kisha kumuingiza mlango wa nyuma wa gari lake na kutoweka naye.

“Sitaki kukumbuka nilivyokuwa najisikia baada ya kukaa zaidi ya saa saba bila kufahamu mtoto wangu wa miezi 18 yupo wapi.”

Hivyo ndiyo anavyoanza kusimulia Maria Sabakuki aliyempoteza mtoto wake wa kiume kwa saa nane.

“Kila nikikumbuka siku ile huwa nalia, sijui asingepatikana ingekuwaje, ”anasema Maria huku akifuta machozi na akicheza cheza na kijana wake mikononi.

“Nilimaliza kufua kama saa nne kasorobo, nikaenda barazani nimchukue mtoto nije kumuogesha, hapo ndipo maisha yangu yaliposimama kwa muda, hakuwepo na watoto wengine hawakuwepo pia, kila niliyemuuliza miongoni mwa wapangaji wenzangu mwanae alikuwa ndani...hakika nilipagawa .

“Nilizunguka mitaa bila kujua namtafuta mtoto ambaye hata jina lake hawezi kulitamka vizuri, nilitoa matangazo kila kona nikiwafahamisha watu mtoto wangu anavyofanana, wapo waliosema nitembee na picha lakini niliamini nikirudi nyumbani atazidi kupotea, ”anasema.

Anasema alisahau kuwa asubuhi wifi yake alifika nyumbani kwake kuchukua mzigo kutoka kwa mumewe na ndiyo aliondoka na mtoto bila kufanya mawasiliano.

Hii ni mifano ya wazazi wawili wanaoteseka hadi leo wakikumbuka matukio ya watoto wao kutoweka.

Matukio ya watoto kupotea yanazidi kushika kasi na polisi wanalitambua hilo kwa mujibu wa takwimu zao ndani ya miaka mitatu watoto 399 wamepotea katika maeneo mbalimbali nchini.

Matukio hayo ni yale tu yaliyoripotiwa vituo vya polisi katika mikoa mbalimbali kati ya Januari mwaka 2016 hadi Agosti mwaka 2018.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa kati ya watoto hao waliopotea wa kiume ni 238 na wa kike 161.

Zinafafanua zaidi kuwa kwa kipindi cha mwaka 2016 watoto 186 waliibwa, kati ya hao wanaume ni 114 na wanawake 72.

Ripoti hiyo inaitaja mikoa inayoongoza kwa wizi wa watoto kwa mwaka huo kuwa ni Dar es Salaam watoto 23 (Temeke 13, Kinondoni 10) na Shinyanga watoto 22, Mara watoto 16, Mbeya 15 na Morogoro 13.

Mwaka 2017 jumla ya watoto 134 waliibwa wakiwamo wanaume 79 na wanawake 55 na mkoa ulioongoza kwa matukio hayo ni Dar es Salaam watoto 23 (Kinondoni 13, Ilala sita na Temeke wanne), ukifuatiwa na Kilimanjaro ambako kuliripotiwa kuibwa watoto 15, Manyara 13 na Shinyanga 11.

Takwimu hizo zinaonyesha kwa mwaka 2018 kuanzia Januari hadi Agosti watoto walioripotiwa kuibwa ni 79 ambao kati yao wanaume ni 45 na wanawake 34.

Mikoa iliyoongoza kwa mwaka 2018 ni Mwanza watoto 11, Geita wanane na Dar es Salaam wanane (Ilala watano, Kinondoni watatu).

Alisema kati ya watoto 399 walioibwa, 209 walipatikana. Mwaka 2016 walipatikana 91, mwaka 2017, 71 na mwaka 2018, 47.

Mbali ya takwimu hizo kuonyesha watoto waliopotea pia zimeonyesha watuhumiwa wa wizi wa watoto waliokamatwa ni 186 katika kipindi cha miaka mitatu.

Ilisema mwaka 2016 walikamatwa watuhumiwa 81 waliohusika na matukio hayo, mwaka 2017, walikamatwa 65 na mwaka 2018 walikamatwa 40.

Kulingana na takwimu hizo inaonyesha robo tatu ya watoto wanaopotea ni wa kiume.

Kwa mujibu wa Shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF ilieleza kuwa takribani watoto 1.2 milioni husafirishwa kutoka nchi moja kwenda nyingine kila mwaka.

“Familia hazifahamu madhara ya kusafirisha watoto, huamini wanakwenda kupata unafuu wa maisha na kuajiriwa kwenye kazi bora zaidi na kuishi nje ya nchi, ”ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Mbali ya mataifa ya Afrika yapo mataifa mengine yanayopambana na changamoto ya watoto kupotea ikiwamo Australia, ambako inakadiriwa watoto 20,000 hupotea kila mwaka.

Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya Australian Federal Police, National Coordination Centre.

Ilisema mwaka 2016 walikamatwa watuhumiwa 81 waliohusika na matukio hayo, mwaka 2017, walikamatwa 65 na mwaka 2018 walikamatwa 40.

Saa tatu za awali

Inaelezwa kuwa saa tatu za awali ni muhimu zaidi unapotokea utekaji wa mtoto kwa kuwa takwimu zinaonyesha asilimia 76.2 ya watoto waliuawa ndani ya saa tatu katika matukio ya utekaji.

Saa mbili za taharuki

Inaelezwa kuwa humchukua mzazi saa mbili kupata akili ya kutoa taarifa ya kupotelewa na mtoto kutokana na kupatwa na taharuki.



Chanzo: mwananchi.co.tz