HALMASHAURI ya wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, imewafukuza kazi watumishi sita waliosababisha halmashauri hiyo kupata hati yenye mashaka kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa kipindi cha mwaka wa fedha ulioishia Juni, 2020.
Watumishi hao ni kutoka Idara ya fedha na manunuzi, ambapo pia panoja na adhabu hiyo watakatwa fedha kwenye mishahara yao.
Akiwasilisha taarifa katika kikao cha kujadili taarifa ya CAG, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Ndaki Mhuli, amesema hati hiyo yenye mashaka imesababishwa na kukusanywa kwa maduhuli yenye thamani ya milioni 112.5 lakini fedha hizo hazikupelekwa benki.
Mhuli amesema, sababu nyingine ni kufanya marekekibisho kwenye mfumo wa fedha (LGRCIA), bila kupata idhini kutoka kwa Afisa Masuhuli yenye thamani ya sh. milioni 624.1.
“Pia yapo matumizi yaliyofanyika bila kuwa na viambatanisho yenye thamani ya milioni 101.5, kukosekana kwa hati ya malipo ya milioni 59.2 wakati wa ukaguzi pamoja na kukosekana kwa viambatanisho vya milioni 10 kwenye ujenzi wa madarasa kupitia akaunti ya kijiji cha Ngarenairobi” amesema Mhuli.
Katika taarifa hiyo ya CAG, hoja 197 zimeibuliwa, ambapo katika mwaka wa fedha 2019/2020 zipo hoja 71 na hoja za miaka ya nyuma 2018/2019 kurudi nyuma zipo hoja 125.