Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais wa Taffa kuagwa kesho Karimjee, kuzikwa J’mosi

Wed, 13 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mwili wa aliyekuwa, Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (Taffa), Stephen Ngatunga unatarajia kuagwa kesho Alhamisi Machi 14, 2019 katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa bodi ya Taffa, Otieno Igogo akizungumza na Mwananchi jana Jumanne Machi 12, 2019 alisema baada ya mwili kuagwa katika viwanja hivyo, utasafirishwa siku hiyo hiyo kwenda katika Kijiji la Lituhi, wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma ambako mazishi yatafanyika Jumamosi, Machi 16, 2019.

 “Tunatarajia kumuaga mwenzetu Alhamisi ya wiki hii, katika viwanja vya Karimjee kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 8 mchana na baada ya hapo mwili utasafirishwa kwenda kijiji cha Lituhi  huko kwa ajili ya mazishi,” alisema Igogo.

Ngatunga alifariki Jumatatu iliyopita Machi 11, 2019 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), alikokuwa anapatiwa matibabu baada ya kuugua kwa muda mfupi.

“Ngatunga ameugua kwa muda mfupi sana, kwani wiki iliyopita alikuwa Dodoma kikazi, alikuwa ameitwa na uongozi wa juu ili kwenda kutoa maoni yetu sisi kama wana tasnia wa forodha kuhusiana na sheria zinazobadilishwa zinazohusu usimamizi wa shughuli zetu,” alisema Igogo.

“Alivyorudi kutoka huko, alikuwa hayuko vizuri kiafya hivyo alilazwa Hospitali ya Burhani kwa siku moja na Jumamosi ya Machi 9, 2019, hali yake ilibadilika na kukimbizwa Muhimbili kwa ajili ya matibabu, hivyo hadi anafikwa na mauti alikuwa bado anapatiwa matibabu Muhimbili,” alisema Igogo.

Alisema Ngatunga alichaguliwa kuwa rais wa Taffa, mwaka 2015 na alitarajia kung’atuka madarakani Aprili 2019 ambapo Taffa ilikuwa inatarajia kufanya uchaguzi.

“Kampuni zaidi ya 600 zenye wafanyakazi zaidi ya 10,000 wa Forodha wanatarajia kushiriki shughuli za kumuaga Ngatunga katika Viwanja vya Karimjee” alisema Igogo.

Kwa upande wake, Katibu wa Bodi ya Wadhamini wa Taffa, Rukia Shamte alisema shughuli za Forodha zitasimama kwa muda siku hiyo ili kupisha shughuli ya kumuaga Ngatuga. Marehemu ameacha mke na watoto watano na kwa sasa msiba upo nyumbani kwa marehemu, Mtoni Kijichi.



Chanzo: mwananchi.co.tz