Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mhe Dk Samia Suluhu Hassan, imeridhia kugawa eneo la kilomita za mraba 194 la pori tengefu la Mto Umba kwa Wananchi wa Vijiji vinne vya Mkota, Mwakijembe, Mbuta na Pelani vilivyopo Wilayani Mkinga Mkoa wa Tanga.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa (@jerrysilaa ) amesema hayo katika mkutano wa Wananchi uliofanyika katika Kijiji cha Mwakijembe Wilayani Mkinga.
Silaa ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri Nane wa Kisekta wanaosimamia maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusu utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi ya Vijiji 975 Nchini amesema Rais Dk Samia amegawa eneo hilo kwa Wananchi kwa ajili ya matumizi ya Vijiji, ili wanaoishi katika maeneo hayo waweze kunufaika kupitia shughuli zao za kiuchumi na kijamii.
Amewaonya Viongozi katika ngazi za msingi kwenye Vijiji na Kata husika, wasithubutu kuihujumu ardhi inayopaswa kugawiwa kwa wananchi na badala yake kujinufaisha binafsi.