Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Raia wa Uturuki agongwa na gari katika ujenzi wa SGR

Tue, 4 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Raia wa Uturuki Adem Demir mfanyakazi katika kampuni ya Yapi Markez inayoshughulika na utengenezaji wa reli ya kisasa (SGR) amefariki dunia kwa kugongwa na gari la kampuni hiyo.

Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Wilbroad Mutafungwa akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Juni 3, 2019 amesema tukio hilo lilitokea jana Jumapili Juni 2, 2019 majira ya saa 5.45 usiku huko eneo la Mkambarani  ndani ya kambi ya  ujenzi wa SGR.

Amesema raia huyo aligongwa na gari aina ya Man TGS Tipper mali ya kampuni ya Yapi iliokuwa ikiendeshwa na  dereva Andrea.

Kamanda huyo amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva huyo kutokuwa mwangalifu wakati akiendesha gari hilo ambalo lilikuwa limebeba kifusi cha udongo wakati akijiandaa kushusha.

Amesema dereva wa gari hilo amekamatwa huku mwili wa marehemu umefanyiwa  uchunguzi katika hospitali ya mkoa wa Morogoro na kukabidhiwa kwa ndugu zake kwaajili ya taratibu za kusafirisha kwenda nchini Uturuki kwa ajili ya Mazishi.

Naye mkuu wa mkoa wa Morogoro Dk Steven Kebwe  ameagiza kambi zote zinazofanya shughuli za ujenzi usiku na mchana kuhakikisha kunakuwa na taa na ulinzi wa kutosha na usalama.

Pia Soma

“Huyo raia aliyegongwa ni mfanyakazi wa kampuni hiyo ya ujenzi wa reli ya mwendo kasi ya Yap Markez, na alikuwa akielekeza gari hiyo ya mchanga sehemu ya kumwaga kifusi lakini kwa bahati mbaya eneo hilo hakukuwa na taa za kutosha,” amesema

Amesema gari hilo lilimgonga sehemu ya mguu na kuanguka chini kisha kugongwa sehemu yake ya paja na kusababisha kifo.

Mkuu huyo wa mkoa ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama amesema mtumishi huyo aliyefariki hata tochi aliokuwa akitumia ilikuwa na mwanga hafifu hivyo kusababisha dereva huyo kutoona vizuri nyuma yake na hivyo kusababisha ajali hiyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz