Morogoro. Imelda Milanzi, rafiki wa Jasmin Ngole mwanafunzi aliyejiua kwa kujipiga risasi kooni na kufumua sehemu ya utosi, ameweza kufika shuleni na kuendelea na masomo huku hali yake ya afya ikiwa imeimarika.
Baada ya kifo cha rafiki yake Imelda ambaye anasoma kidato cha nne katika shule ya sekondari Lupanga alishindwa kwenda shule kwa siku nne hivyo kushindwa kufanya mitihani ya mwezi.
Mitihani hiyo ya mwezi ilifanyika Februari 22,2019 siku moja baada ya mazishi ya rafiki yake ambapo alishindwa kufanya mitihani hiyo baada ya kuishiwa nguvu na kulia wakati wote.
Mwili wa Jasmin ulikutwa kando ya barabara nyembamba, eneo la Kola B Manispaa ya Morogoro, alfajiri ya Februari 19, 2019 huku bastola aliyotumia kujiua, mali ya Profesa Hamis Maige iliyokuwa na magazine moja na ganda la risasi vikiwa kando yake.
Akizungumzia na Mwananchi leo Jumanne Februari 26,2019 hali ya mwanafunzi huyo makamu mkuu wa shule hiyo, Daud Masunga amesema Imelda ameweza kufika shuleni hapo na ameendelea na masomo kama kawaida.
Masunga amesema walimu wameendelea kumpa ushauri nasaha ili aweze kuona tukio limeshapita na kumtaka asome ili aweze kufanya mitihani yake ya kumaliza kidato cha nne mwishoni mwa mwaka.
Soma Zaidi: VIDEO: Mapya yamfika rafiki wa mwanafunzi aliyejiua kwa risasi
"Mkasa uliompata ni mkubwa hasa ukizingatia umri wake bado mdogo, walimu tuko naye karibu kwa kumpa ushauri na nasaha ili arudi kwenye hali ya kawaida na tunashukuru sasa hivi yuko vizuri na ameanza kuchangamka," amesema Masunga.
Kwa upande wake Imelda amesema anaendelea vizuri na amemshukuru Mungu kwa mkasa uliompata na kwa sasa anajiandaa na mitihani japokuwa kuna wakati huwa anamkumbuka rafiki yake.
Soma Zaidi: VIDEO: Mwanafunzi aliyejipiga risasi alivyomaliza siku yake ya mwisho duniani