VIJANA wawili wamekufa baada ya kupigwa na radi walipokuwa wanachunga mifugo wakati mvua inanyesha katika Kijiji cha Utenge Kata ya Nsenda wilayani Urambo mkoani Tabora.
Akizungumza jana, Diwani wa Kata ya Nsenda, Erasto Mahona amesema tukio hilo lilitokea Novemba 26, mwaka huu wakati vijana hao wakichunga mifugo na kisha kujificha kwenye mti.
Amesema maafa hayo yalitokea katika Kijiji cha Utenge Kitongoji cha Mkola Kata ya Nsenda Tarafa ya Urambo Wilaya ya Urambo mkoani hapa muda wa saa 11:00 jioni.
Vijana hao waliomaliza darasa la saba mwaka huu katika Shule ya Msingi Mkola walikuwa wamefaulu kuendelea na kidato cha kwanza mwakani. Walipata alama C kila mmoja.
Amewataja vijana hao kuwa ni Hamisi Juma na Amani Paulo wote wakiwa na miaka 19. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amekiri kutokea kwa tukio hilo.
Hili ni tukio la tatu la watu kuuawa na radi ambapo Machi 15, mwaka huu mkazi wa Kijiji cha Jionee Kata ya Songambele wilayani humo, Matomolo Michael alipigwa na radi na kufa papo hapo alipokuwa akichochea moto kwenye bani la tumbaku.
Pia katika Kata ya Imalamakoye, mjasiriamali Josephina Saidi alikufa baada ya kupigwa na radi alipokuwa mgahawani kwake.