Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Radi yaua watoto 2, yajeruhi wazazi

30ada6288dd99a15ad0eec2c69e6878a Radi yaua watoto 2, yajeruhi wazazi

Sat, 19 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

RADI imeua watoto wawili wa familia moja na kujeruhi wazazi katika Kijiji Cha Shasya Kata ya Halungu wilayani Mbozi Mkoa wa Songwe .

Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Wizman Mwashibanda alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 8:00 mchana.

Alisema baada ya kusikia sauti kubwa ya radi, alifika haraka eneo la tukio na kukuta watoto wawili, Miznala Mgale (4) na dada yake, Edna Mgale(14) wakiwa tayari wamepoteza maisha katika vyumba tofauti. Mama wa watoto hao alikuwa amejeruhiwa na kupoteza fahamu jikoni.

Alisema siku iliyofuata watoto hao walizikwa. Mama yao anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Mbozi Misheni alikokimbizwa baada ya tukio hilo.

Akizungumzia tukio hilo, baba wa watoto hao waliopoteza maisha, Mawazo Mgale, alisema lilitokea ghafla na radi ilipiga vyumba vyote vitatu vya nyumba yake. Alisema yeye alikuwa sebuleni na mtoto wake, Miznala aliyefariki hapo hapo.

Alisema Edna alikuwa kwenye chumba kingine, ambapo naye alifariki hapo hapo. Mama yao aliyekuwa jikoni, alijeruhiwa vibaya.

"Mimi baada ya tukio hilo miguu yote ilikufa ganzi, lakini baada ya muda mwili ulirudi katika hali yake ya kawaida," alisema Mawazo.

Diwani wa Kata hiyo ya Halungu, Maarifa Mwashitete alisema tukio hilo limewashitua na kuwasikitisha. Alisema hiyo ni mara ya kwanza kwa matukio ya aina hiyo kutokea katika kata hiyo.

HabariLEO ilipomhoji Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, George Kyando alikiri kupokea taarifa za tukio hilo. Alisema kuwa tayari kikosi kazi cha wilaya ya Mbozi, kinafuatilia suaha hilo kwa undani na atatoa taarifa.

Chanzo: habarileo.co.tz