Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Radi yaua mwanafunzi mmoja, 22 wajeruhiwa

45177 Pic+radi Radi yaua mwanafunzi mmoja, 22 wajeruhiwa

Thu, 7 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mtwara. Mwanafunzi mmoja wa shule ya sekondari Mikindani Manispaa ya Mtwara Mikindani, Abdul Masamba amepoteza maisha baada ya kupigwa na radi wakati akiwa shuleni huku wenzake 22 wakijeruhiwa.

Tukio hilo limetokea jana ambapo kulikuwa na hali ya mawingu na radi.

Akizungumza na waandishi wa habari, mkuu wa wilaya ya Mtwara, Evod Mmanda amesema wanafunzi waliojeruhiwa na radi hiyo wamepatiwa huduma za awali katika Zahanati ya Mikindani na kisha kuhamishiwa katika hospitali ya rufaa ya Ligula.

“Hapa Ligula sasa hivi tuna wagonjwa 22, wawili walitibiwa wakaondoka, wavulana wako saba na wasichana 15 wamelazwa hapa wanaendelea kupatiwa huduma na katika tukio hili kwa bahati mbaya tumempoteza mwanafunzi mmoja ambaye alikufa kwenye tukio,” alisema Mmanda.

Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Ligula, Dk Lobikieli Kisambu amesema wanafunzi hao wanaendelea kupatiwa matibabu nakwamba msichana mmoja na mvulana ndio wanaoonekana kuwa na majeraha makubwa.

“Wanafunzi saba wa kiume tumewalaza wodini, kati yao sita tumewaweka kwa ajili ya mapumziko na mmoja hali yake kidogo sio nzuri lakini naye anaendelea na matibabu.”

“Kwa wasichana tumewapeleka wodini wote na mmoja ndio kidogo anaonekana  kuwa na majeraha lakini wote wanaendelea na matibabu.”

“Mmoja wa kiume bado tunaye hapa emergency (dharura) anaendelea kupatiwa matibabu kwa sababu alikuja mwishoni lakini bado hali yake kidogo sio nzuri na wawili waliruhusiwa kwa sababu hali zao zilikuwa nzuri,” amesema Kisambu.

Mwalimu wa shule hiyo, Elizabeth Moses amesema radi hiyo ilipiga baada ya mawingu mazito kutanda na baada ya dakika tano ilipiga radi nyingine na kusababisha wanafunzi kuanza kupiga kelele.

“Tulifika kwenye darasa la kidato cha tatu A tukakuta wanafunzi wengi wamelala chini na kulikuwapo na mwalimu darasani kwa hiyo tukaanza kuwatoa na kuwakimbiza zahanati na majirani walikuja kusaidia pamoja na watumishi wa ofisi za wilaya na mkoa walitusaidia,” amesema Mwalimu Moses.



Chanzo: mwananchi.co.tz