Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RUWASA yatia saini mikataba 15 ujenzi miundombinu ya maji

Makongoro Pc 660x400.jpeg Mkuu wa Mkoa, Makongoro Nyerere

Mon, 6 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakazi 24,129 wa vijiji 14 vya Mkoa wa Manyara, wanatarajia kunufaika na huduma ya majisafi, baada ya Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA), kutia saini mikataba 15 na makandarasi wa kujenga miundombinu ya maji.

Mkuu wa Mkoa huo Makongoro Nyerere, alisema katika utekelezaji wa miradi hiyo, vijiji 14 ndiyo vitaanza kuguswa ili kupunguza adha hiyo ya maji.

Makongoro aliyasema hayo wakati akizungumza na wakuu wa wilaya, wafanyakazi wa RUWASA na makandarasi waliopewa zabuni za kujenga miradi ya maji na wengine kusambaza vifaa vya ujenzi.

“Mkoa wetu kwa mwaka wa fedha 2022/2023, umeidhinishiwa shilingi bilioni 15.406 kutoka vyanzo mbalimbali, ambazo zitatumika kukamilisha miradi 28 inayoendelea, kujenga miradi saba mipya, kuongeza mtandao miradi nane, kuchimba visima 26 na kufanya usanifu wa miradi 53.

“Miradi hiyo itasogeza huduma ya maji kwenye vijiji vipya 40 kwa hiyo ifikapo Desemba mwaka huu idadi ya vijiji ambavyo havina huduma ya uhakika itapungua kutoka vijiji 91 hadi vijiji 51.

"Wazabuni ambao mmepewa kazi ya kusambaza vifaa vya ujenzi wa miradi hakikisheni mnasambaza vifaa vyenye ubora na vifaa vitapimwa ubora wake hivyo vifaa viwe vizuri visiwe na doa," alisema Makongoro.

Awali, Meneja wa RUWASA mkoani Manyara, Wolta Kirita, wakati akisoma taarifa ya utekelezaji wa shughuli za RUWASA, kuanzia Julai mosi mwaka jana hadi Januari 31, mwaka huu, alisema RUWASA makao makuu, ndio inaratibu ununuzi wa mabomba yote kutoka viwandani na uratibu huo uko katika hatua za mwisho.

Alisema kwa mkoa huo miradi inayonunuliwa mabomba ni Mdunga-Utwari, Einoth-Losinyai, Kiperesa, Esunguta, Aicho, Titiwi, Naberera-Losokonoi-Lorbeno, Orkesumet-Lerumo, Komolo-Olembele na miradi mbalimbali kwa mwaka huu wa fedha inaratibiwa na RUWASA makao makuu.

Alisema ununuzi wa vifaa vya ujenzi na makandarasi wa kujenga miundombinu ya maji unaratibiwa na bodi ya manunuzi ya kanda.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Genuine Limited, ambaye amepewa kandarasi hiyo, Loserian Mollel, alisema wana uwezo, kwamba hawatakuwa wababaishaji bali watafanya kazi kwa muda uliopangwa na kwa viwango.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live