Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RUAHA MKUU KULINDWA KUWEZESHA 15% YA MAJI BWAWA LA UMEME NYERERE

Af6aeff18e488ba4bedeb0fee20fab1c.jpeg RUAHA MKUU KULINDWA KUWEZESHA 15% YA MAJI BWAWA LA UMEME NYERERE

Thu, 25 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

“Wanaofanya shughuli za maendeleo katika vyanzo vinavyotiririsha maji katika Mto Ruaha Mkuu wajiandae kuumia ili kuwezesha mradi mkubwa wa bwawa la kufua umeme wa maji la Julius Nyerere unaojengwa kwenye bonde la mto Rufiji upate maji kwa asilimia 100,” anasema Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Albert Chalamila.

Maji ya mto huo (Mto Ruaha Mkuu) yanatarajia kuchangia asilimia 15 ya maji yote yanayohitajika kufua umeme katika mradi huo wa Julius Nyerere utakaokuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 mara utakapokamilika Juni 2022.

Chalamila anasema shughuli za kibinadamu ikiwemo ukataji wa miti kwa ajili ya mkaa na mbao, kilimo na ufugaji ni baadhi ya sababu zinazotajwa kuharibu mazingira na kutishia usalama wa vyanzo vya maji ya Mto Ruaha Mkuu.

“Kwahiyo tunahitaji kutumia sheria kwa nguvu zetu zote ili asilimia 15 ya maji kutoka katika mto Ruaha Mkuu kwenda Rufiji ipatikane, na hapa wapo watakaoumizwa sana hivyo nitoe rai kwao wawe sehemu ya kuhiifadhi na kulinda vyanzo hivyo,” Chalamila anasema.

Anasema serikali inatambua kwamba wafugaji ni lazima wafuge na wakulima lazima walime, lakini ni lazima wadau hao waendelee kuelimishwa ili ufugaji wao uwe ni wa mifugo michache yenye tija kwa mazingira na kilimo chao kiwe kile kinachozingatia matumizi endelevu ya maji ili yatiririke kuelekea mto Ruaha Mkuu na hatimaye Rufiji.

Msimamizi wa ujenzi wa mradi huo, Mhandisi Dismas Mbote anasema mradi huo utakuwa na bwawa lenye urefu wa kilometa 100 na upana wa kilometa 25 likiwa na uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo wa maji bilioni 33.2 katika kiwango chake cha juu.

Mradi huo ambao awali ulijulikana kwa jina la Stieglers Gorge utakuwa wa kwanza kwa ukubwa Afrika Mashariki na Kati hatua iliyoelezwa na Mhandisi Mbote kwamba itasaidia kupunguza tatizo la nishati hiyo muhimu kiuchumi na kijamii.

Mhandisi huyo anasema hatua ya kuanza kwa mradi huo imekuja baada ya miaka 40 tangu utafiti wa uzalishaji wa umeme katika Mto Rufiji ufanywe wakati wa utawala wa Rais wa Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere.

Anasema ujenzi wa bwawa hilo unaofanywa na wakandarasi kutoka nchini Misri (Arab Contractors and Elsewedy Electric) unatarajiwa kugharimu dola za Marekani bilioni 2.9 sawa na shilingi trilioni 6.5 za Kitanzania.

“Ili uwekezaji wa fedha zote hizi uwe na maana ni lazima mradi huu upate maji ya kutosha. Kwahiyo ni muhimu kwa wadau wote kushirikiana kutunza na kulinda vyanzo vyote vya maji yanayotiririka kuelekea katika mto Rufiji,” anasema.

Mbali na Mto Ruaha Mkuu utakaochangia asilimia 15 ya maji katika mradi huo, Mhandisi Mbote anataja mito mingine itakayochangia maji kuwa ni mto Luwegu asilimia 19, mto Kilombero asilimia 65 na asilimia moja inayobaki ni kutoka katika vyanzo vidogovidogo.

Anasema bwawa la mradi huo litaanza kujazwa mwaka huu baada ya ujenzi wa kingo zake kukamilika na linatarajiwa kujaa kwa asilimia 100 katika kipindi cha miaka mitatu.

“Kwahiyo bwawa hilo linahitaji asilimia 15 ya maji kutoka mto Ruaha Mkuu ambao vyanzo vyake vingi vya maji viko katika mkoa wangu wa Mbeya lakini pia mkoa wa Njombe na Iringa,” anasema Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.

Anasema mto Ruaha Mkuu unaanzia kwenye vyanzo vya maji kwenye mito midogo iliyopo katika mikoa ya Mbeya, Njombe na Iringa; na milima ya Uporoto na Kipengele kisha unakatiza katikati ya hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Kwa kuwa mikoa hiyo yote ni wadau, Chalamila anasema watakuwa na kikao cha ujirani mwema watakachokitumia kuweka mikakati ya pamoja na kuisimamia iliyopo ili kutunza na kuvilinda vyanzo vyote vinavyotirisha maji katika mradi wa umeme wa bwawa la Nyerere.

“Tutakuwa na wajibu wa kuwaondoa wakulima na wafugaji katika vyanzo hivyo na kuhakikisha utaratibu wa matumizi ya maji unakuwa ule unaozuia maji yasipotolee mashambani bila sababu ya msingi na badala yake yatumike na yote yanayobaki yarudi mto Ruaha Mkuu ili kutoathiri mtiririko wake,” anasema.

Mbali na maji yake kutegemewa kwa asilimia 15 kwa ajili ya uzalishaji umeme katika mradi wa umeme wa Nyerere, Chalamila anasema asilimia 80 ya maji ya mto huo ndio yanayotegemewa kwa uzalishaji wa umeme katika mabwawa ya Kidatu na Mtera.

Anasema mtiririko wa maji katika mto huo uliathiriwa sana na shughuli za kilimo na ufugaji katika eneo la Mbarali kwenye eneo oevu la bonde la Ihefu.

“Mipaka ya hifadhi ya Taifa ya Ruaha ilipopanuliwa hadi katika bonde hilo la Ihefu ambalo pia maji yake yanatiririka kuelekea mto Ruaha Mkuu, tuliwaondoa wakulima na wafugaji,” anasema.

Pamoja na kuondolewa Chalamila anasema bado kuna baadhi ya wafugaji wanarudi kinyemela katika eneo hilo na akaagiza mamlaka zinazohusika kuendelea kuchukua hatua kali.

Afisa Mazingira wa Wilaya ya Mbeya, Godwin Gozbera anazungumzia vyanzo vilivyoko katika wilaya yake akisema vingi vipo katika hali nzuri ingawaje baadhi yake vilivamiwa na kutumiwa kwa shughuli za kibinadamu.

Anasema wanavilinda vyanzo hivyo kwa kutumia sheria ya usimamizi wa mazingira namba 20 ya mwaka 2004 inayozuia kufanyika kwa shughuli za kibinadamu mita 60 kutoka katika kingo za vyanzo hivyo.

Mtaalamu wa maji na afisa kidakio cha maji wa bonde la mto Ruaha Mkuu, Abisai Chilunda anasema suala la utunzaji wa rasilimali za maji ni suala mtambuka linaloshirikisha wadau mbalimbali zikiwemo halmashauri pamoja wadau mbalimbali zikiwemo jumuiya za watumiaji maji.

Anasema kazi hiyo inafanywa kwa kutumia Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji Na. 11/2009 inayolenga kuhakikisha kuwa Rasilimali za Maji hapa nchini zinatunzwa, zinatumiwa, zinaendelezwa, zinaboreshwa, zinasimamiwa na kudhibitiwa kwa kuzingatia kanuni zilizopo.

Anasema mtu yeyote anayetaka kuchepusha, kukinga, kuhifadhi, kuchukua na kutumia maji kutoka kwenye chanzo cha maji juu ya ardhi au chini ya ardhi au kujenga miundombinu yeyote lazima aombe kibali cha kutumia maji.

“Mtiririko wa maji katika bonde la mto Ruaha Mkuu ni wa kuridhisha kwasababu vyanzo vingi bado havijaharibiwa, na migogoro ya maji imepungua,” anasema Chilunda na kutaka elimu ya uhifadhi wa vyanzo vya maji iendelee kutolewa.

Akizungumzia changamoto ya uharibifu wa vyanzo na upotevu wa maji, mtaalamu huyo wa maji anasema maji mengi yanapotea katika bonde hilo kwasababu miundombinu mingi ya umwagiliaji haipo vizuri kwani mifereji yake haijasakafiwa.

“Lakini pia mabanio mengi bado yanapoteza maji na kuna baadhi ya wakulina wanachepusha maji kinyume na sheria huku wafugaji wanaendelea kuingiza mifugo yao katika maeneo ya vyanzo,” anasema.

Mmoja wa viongozi wa skimu ya Igomelo, wilayani Mbarali mkoani Mbeya Aman Mdendemi anasema skimu hiyo inayotegemea maji kutoka mto Mbarali; ina zaidi ya hekta 312 zinazolimwa kwa mwaka mzima.

“Ili kupata maji ya kutosha katika mashamba haya tumeanza kusakafia mifereji ya umwagiliaji hatua iliyopunguza upotevu wa maji na tunahakikisha wakulima wanamwagilia maji kwa kiasi kinachohitajika bila kuzidisha kiwango,” anasema na kufafanua kwamba kilometa tatu kati ya tano za skimu hiyo tayari zimesakafiwa.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya watumiaji maji mto mdogo Mkoji, Julius Mwanibingo anasema jumuiya yao imekwishahifadhi vyanzo 25 kati ya zaidi ya 400, Mbeya Vijijini.

Anasema kazi ya kuhifadhi vyanzo hivyo wanafanya kwa kushirikiana na Ofisi ya Bonde la Rufiji wanaowasaidia kuweka bikoni katika vyanzo vya maji ili kutambulisha mipaka yake.

“Vyanzo hivyo vilikuwa vikitumika kulishia mifugo kabla ya kutambuliwa na kuanza kulindwa dhidi ya shughuli zote za kibinadamu,” anasema na kuongeza kwamba ndani ya vyanzo hivyo 25, kuna uoto wa asili wa kutosha, maji na mtiririko wake unaongezeka na wananchi hawaingii tena kufanya shughuli za kibinadamu.

Udhibiti huo anasema umewezesha mtiririko wa maji ya vyanzo hivyo kuelekea mto Ruaha Mkuu kuongezeka hali inayoongeza matumaji ya kupatikana kwa maji ya kutosha katika mto Rufiji kwa ajili ya uzalishaji wa umeme kupitia mradi mkubwa wa Julius Nyerere.

Hatua zote nane (8) za utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa bwawa la kufua umeme wa maji la Julius Nyerere (JNHPP-MW2115) kwenye bonde la mto Rufiji unaendelea kwa kasi inayohitajika, Mhandisi Mbote amewaambia waandishi wa habari kutoka Iringa waliotembelea eneo la mradi hivikaribuni.

Mhandisi Mbote ametaja hatua hizo kuwa ni ujenzi wa njia kubwa ya ardhini ya mchepuko wa maji (diversion tunnel), sehemu ya kufua umeme (power house), ukuta utakaotengeneza bwawa, eneo la kupokelea umeme unapozalishwa (Switch yard), power intake, barabara na madaraja, saddle dams nne na kuchakata mawe yanayotumika kutengeneza zege na mahitaji mengine.

“Mradi huu mkubwa wa umeme una miradi mingi ndani yake na yote iko katika hatua mbalimbali na hatua hizo kama nilivyozitaja kwa pamoja ndiyo zinajenga mradi mmoja wa Julius Nyerere Hydro Power Project Megawati 2115, mafundi wako kazini na wanaendelea na ujenzi kwa kasi kubwa kama inavyohitajika na ifikapo Juni 2022 umeme wake utaingizwa katika gridi ya Taifa kwa matumizi ya nchi.” anasema.

Anasema kukamilika kwa mradi huo kutawezesha uanzishwaji wa miradi ya kilimo cha umwagiliaji kwenye eneo la chini la mradi, kudhibiti mafuriko kwenye eneo la chini la mto Rufiji, kuongeza usambazaji wa maji kwa ajili ya matumizi ya majumbani, kuanzisha utalii wa kupiga picha, uvuvi na safari za boti kwenye eneo la bwawa na kuongeza udhibiti na uhifadhi wa wanyama dhidi ya majangili.

Anasema jambo la kufurahisha tayari mradi umeanza kuchangamsha uchumi wa nchi na kutolea mfano wazalishaji wa vifaa mbalimbali vya ujenzi kama nondo na sementi wanavyonufaika nao.

Anasema zaidi ya watanzania 8,000 kutoka maeneo mbalimbali nchini hususan yale yanayozunguka eneo la mradi wameajiriwa na wanashiriki katika mradi kwa ari kubwa.

Kwa upande wao, wakazi wa kijiji cha Kisaki kilomita 60 kutoka eneo la mradi wamempongeza Rais Dk John Magufuli kwa kuwaletea mradi huo kwani tayari manufaa yake wameanza kuyaona.

“Kisaki inakuja juu, kuna nyumba za kisasa za kulala wageni na biashara mbalimbali zinafanyika kwa kasi kubwa kutokana na ongezeko la wageni wanaopita hapa wakielekea katika mradi huo,” anasema Juma Ubwaa mmoja wa wakazi wa kijiji hicho.

Ubwaa anasema wana uhakika mradi ukimalizika Kisaki utakuwa mji mkubwa wenye muingiliano mkubwa wa shughuli za kibinadamu na hivyo kusukuma zaidi maendeleo yake na watu wake.

Naye mwanakijiji mwingine Asha Juma anasema wana uhakika mradi huo utachochea pia ujenzi wa barabara nzuri kutoka Morogoro na hivyo kuongeza wageni wengi Kisaki na kuchochea shughuli za kilimo na biashara.

Chanzo: habarileo.co.tz