Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RTO aliyeshushwa cheo na Lugola awatupia lawama Tanroads ajali za barabarani Mbeya

Sat, 21 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Aliyekuwa kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani (RTO) Mkoa wa Mbeya, Leopord Fungu amewatupia lawama Wakala wa Barabara (Tanroads) kuwa ndiyo chanzo cha ajali mkoani hapa kutokana na miundombinu ya barabara kuwa mibovu.

Hata hivyo, kaimu meneja wa Tanroads mkoani hapa, Eliazary Rweikiza amejibu madai hayo akisema chanzo cha ajali ni magari mabovu ambayo wamiliki wake wamekuwa hawana uangalizi wa karibu kabla ya kuyaruhusu kuanza safari.

Jana, Fungu aliyeshushwa cheo na waziri mpya wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kutoka kuwa mrakibu wa polisi hadi mrakibu msaidizi alijitokeza kwenye mkutano wa madereva wa bajaji na bodaboda jijini Mbeya, uliokuwa umelenga kujitambulisha kwa RTO mpya, Jumanne Mkwama na Fungu kuwaaga madereva hao

Katika mkutano huo uliofanyika Uwanja wa FFU, Fungu alisema Tanroads imekuwa chanzo cha ajali kutokana mkoa kuwa na barabara mbovu pamoja na ukosefu wa alama muhimu za barabarani.

“Asilimia kubwa Mkoa wa Mbeya barabara zake ni mbovu zimejaa mashimo lakini pia ni nyembamba, Kikosi cha Usalama Barabarani tumekuwa tukipiga kelele juu ya kuboresha miundombinu hiyo, lakini utekelezaji wake umekuwa ni wa kusuasua na hata alama za barabarani zimeanza kuwekwa baada ya kufululiza matukio ya ajali,” alisema.

Aliongeza kuwa usalama barabarani ni suala mtambuka, hivyo kila mtu anapaswa kuwajibika kwa nafasi yake ili kuepusha ajali kwani bila kujenga barabara za ziada kwenye miteremko mikali itakuwa ni sawa na bure.

Fungu ametumikia kikosi hicho mkoani hapa kwa miezi sita kabla ya kushushwa cheo mwanzoni mwa mwezi huu kwa kile kilichoelezwa kuwa ameshindwa kusimamia wajibu wake.

Utetezi wa Tanroads

Kaimu meneja wa Tanroads Mkoa wa Mbeya, Rweikiza alisema tatizo kubwa ni ubovu wa magari.

“Barabara zetu zipo katika viwango vinavyostahili, lakini pia kwenye barabara zetu zote tumeweka alama za kuongoza madereva. Hata hivyo mkoa wetu wa Mbeya upo kwenye miinuko mikali na mabonde, hivyo tunakosa sehemu za kujenga za ziada,” alisema Rweikiza.

Rweikiza alisema kutokana na ajali hizo, Serikali ina mpango wa kujenga njia ya mchepuko kutoka Uyole hadi Mbalizi ambayo itakuwa rasmi kwa ajili ya magari ya mizigo yanayokwenda nchi jirani na yale yanayoingia mkoani hapa.

Kamanda mpya wa kikosi hicho, Mkwama alisema bajaji hazitaruhusiwa kupita kwenye barabara kuu ikiwa ni pamoja na kutobeba abiria zaidi ya watatu.

“Ili kuondoa msongamano mjini na (kupunguza) ajali, kuanzia leo (jana) bajaji haziruhusiwi kupita barabara kuu na kubeba abiria zaidi ya watatu kwenye bajaji moja tutakayemkamata hatua kali za kisheria zitachukuliwa juu yake ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani,” alisema.

Mkoa wa Mbeya umekumbwa na jinamizi la ajali baada ya watu zaidi ya 40 kufariki dunia katika kipindi cha Juni na Julai.

Chanzo: mwananchi.co.tz